Dimba

Ukuta wa chuma: Mizinga ya Man City ilivyoshindwa kupenya Arsenal

Na MASHIRIKA September 24th, 2024 2 min read

MARA ya mwisho kwa Inter Milan kujizolea taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ilikuwa 2009-10 wakinolewa na kocha Jose Mourinho aliyewaongoza kupepeta Bayern Munich 2-0 kwenye fainali iliyochezewa jijini Madrid, Uhispania.

Katika safari ya kutinga fainali hiyo, walidengua waliokuwa mabingwa watetezi Barcelona kwa jumla ya mabao 3-2 kwenye hatua ya nusu-fainali. Inter ya Mourinho ilikung’uta Barcelona ya mkufunzi Pep Guardiola 3-1 nyumbani kabla ya kukubali kichapo cha 1-0 katika mkondo wa pili ugenini.

Kwenye mchuano wa marudiano, Mourinho alipanga ‘basi’ sawa na lile lililoshuhudiwa na Guardiola kwa mara nyingine wikendi jana – miaka 14 baadaye – waajiri wake Manchester City walipoalika Arsenal kwa pambano la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Etihad.

Baada ya Leandro Trossard kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza, Arsenal walilazimika kutegemea zaidi maarifa ya Riccardo Calafiori, Gabriel Magalhaes, William Saliba na Jurrien Timber kuunda ukuta wa ‘vyuma na saruji’ ambao ulidhibiti vilivyo makombora makali waliyorushiwa na Man-City.

Kocha Mikel Arteta aliwaleta pia uwanjani mabeki Ben White, Jakub Kiwior na Myles Lewis-Skelly mwishoni mwa kipindi cha pili na wakashirikiana vyema na viungo Thomas Partey na Declan Rice kuibana kabisa safu ya Arsenal walioondoka Etihad na alama moja muhimu kufuatia sare ya 2-2 dhidi ya mabingwa hao watetezi wa EPL.

Isingalikuwa hatua ya refa Michael Oliver kumfurusha Trossard uwanjani na hata kupitiliza dakika alizoongeza mwishoni mwa kipindi cha pili, Arsenal wangaliibuka washindi wa gozi hilo na kutua kileleni mwa jedwali la EPL. Kwa sasa wanakamata nafasi ya nne kwa alama 11, moja nyuma ya Aston Villa na Liverpool. Man-City wanaselelea kileleni kwa pointi 13 kutokana na mechi tano.

Baada ya kulemewa na ukuta wa Maicon Douglas, Lucimar Lucio, Walter Samuel, Javier Zanetti, Thiago Motta, Esteban Cambiasso na Wesley Sneijder mnamo Aprili 2010, Barcelona walisubiri hadi dakika ya 84 kufungiwa na beki Gerard Pique.

Guardiola alirejeshewa kumbukumbu ya mechi hiyo Jumapili baada ya Man-City kusubiri hadi dakika ya 98 kufungiwa bao la kusawazisha na difenda John Stones aliyenyima Arsenal ya Arteta fursa ya kuendeleza ubabe wao dhidi ya miamba hao.

Walipokutana katika EPL msimu uliopita wa 2023-24, Arsenal walishinda Man-City 1-0 mkondo wa kwanza ugani Emirates kabla ya kuagana 0-0 kwenye marudiano Etihad.

Man-City walifungua kampeni za EPL muhula huu kwa kutandika Chelsea 2-0 kabla ya kukomoa Ipswich (4-1), West Ham United (3-1) na Brentford (2-1). Arsenal nao walipepeta Wolverhampton Wanderers 2-0 kabla ya kulaza Aston Villa 2-0 kisha kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Brighton na kupiga Tottenham Hotspur 1-0.

Pamoja na kuwapa mashabiki kitu kipya zaidi cha kufuatilia, Arsenal wanatarajiwa kusalia kuwa wagombezi halisi wa taji la EPL kwa msimu wa tatu mfululizo. Matokeo yao dhidi ya Man-City tangu Januari 2023 ni ithibati tosha kuwa ni miongoni mwa vikosi vinavyojivunia safu bora zaidi za ulinzi duniani kwa sasa.

Baada ya Man-City kuwapiga 1-0 kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA mwanzoni mwa 2023 uwanjani Etihad, Arsenal walifunga watani wao hao penalti 4-1 kufuatia sare ya 1-1 kwenye kipute cha Community Shield mnamo Agosti 2023 ugani Wembley.