Kimataifa

Utawala wa Suluhu wakemewa kufuatia mauaji na kuhangaishwa kwa wapinzani Tanzania

Na MASHIRIKA September 24th, 2024 2 min read

DAR ES SALAAM, TANZANIA

VIONGOZI wakuu wa upinzani nchini Tanzania Jumatatu walikamatwa saa chache baada ya kuongoza maandamano ya kulaani visa vya mauaji na kutekwa nyara kwa wafuasi wao.

Miongoni mwa waliokamatwa ni mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe na naibu wake Tundu Lissu huku polisi wa kupambana na fujo wakitumwa kushika doria katika barabara kadhaa jijini Dar es Salaam kuzuia mikusanyiko ya wafuasi chama hicho.

Bw Lissu alikamatwa asubuhi nyumbani kwake katika kitongoji cha Tegeta, jijini Dar es Salaam saa chache kabla ya maandamano hayo kuanza.

Wakili wa Chadema Hekima Mwasipu alithibitisha kukamatwa kwa Lissu na kusema kuwa alipelekwa katika kituo cha polisi cha Mbweni.

“Ninaelekea katika kituo cha polisi ili kufahamishwa sababu za kukamatwa kwake na viongozi wetu wengine,” Bw Mwasipu akawaambia wanahabari.

Duru zilisema kuwa Bw Lissu alikamatwa majira ya asubuhi nyumbani kwake katika kitongoji cha Tegeta, jijini Dar es Salam saa chache kabla ya wakati ambapo maandamano hayo yaliratibiwa kuanza.

Awali chama cha Chadema kiliapa kuendelea na maandamano hayo licha ya kupigwa marufuku na serikali.

“Ni haki yetu ya kikatiba kufanya maandamano. Lakini tunashangazwa na kiwango cha nguvu ambazo polisi wanatumia kutisha wafuasi wetu na kuhujumu uhuru wetu,” Bw Mbowe akawaambia wafuasi wa Chadema kabla ya kuchukuliwa na polisi, kulingana na video iliyowekwa na chama hicho mitandaoni.

Chadema inaukashifu utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulirejesha Tanzania katika enzi za udhalimu za mtangulizi wake marehemu John Pombe Magufuli.

Mama Samia alichukua hatamu zao uongozi wa nchi hiyo baada ya kifo cha ghafla za Magufuli mnamo Machi 20, 2021.

Awali, alionekana kufungua ukurasa mpya wa uongozi kwa kuondoa vikwazo dhidi ya upinzani na vyombo vya habari.

Aidha, Rais Samia aliamua mawanda ya kidemokrasia kwa kuruhusu viongozi wa upinzani kuendeshwa shughuli zao bila kuingiliwa na serikali.

Lakini chama cha Chadema kinalalamika kuwa katika siku za hivi karibu maafisa wa usalama wamehusika katika visa vya kutekwa nyara kwa wanachama wake kadhaa.

Aidha, viongozi wa chama hicho wanaelekeza kidole cha lawama kwa polisi kufuatia kuuawa kwa mmoja wa maafisa wake Ali Mohamed Kibao.

Bw Kibao, ambaye alihudumu kama Sekritariati ya kitaifa ya Chadema, alitekwa nyara na kisha akapatikana ameuawa mapema mwezi huu wa Septemba.

Mnamo Agosti mwaka huu, polisi waliwakamata viongozi wa chama hicho wakiwemo Mbowe na Lissu, baada ya kutibua mkutano mmoja wa vijana wafuasi wa Chadema.

Makundi ya kutetea haki na serikali za mataifa ya Magharibi, ikiwemo Amerika, yameibua hofu kuhusu kurejelewa kwa visa vya dhuluma kuelekea chaguzi wa serikali za wilaya Novemba mwaka mkuu mwishoni mwa 2025.

Bw Lissu amewahi kukamatwa mara nyingi na mnamo 2017 alipigwa risasi mara kadhaa katika kile kilichotajwa kama jaribio la kumuua.