Jamvi La Siasa

Si mteremko kumtimua Gachagua inavyodhaniwa, hizi hapa sababu

Na CHARLES WASONGA September 25th, 2024 2 min read

HUKU gumzo kuhusu kuwasilishwa kwa hoja ya kumtimua afisini Naibu Rais Rigathi Gachagua, kibarua hicho sio rahisi inavyotajwa kwenye majukwaa ya kisiasa.

Mchakato huo ni changamano kwani ni sawa na ule unaofuatwa katika hoja ya kumwondoa afisini Rais, kwa mujibu wa vipengele vya 144 na 145 vya katiba ya sasa.

Kwa mujibu wa kipengele cha 150 cha Katiba hoja ya kumtimua Naibu Rais sharti iungwe mkono na angalau thuluthi moja ya wabunge, yaani wabunge 117 kati ya 349, ndiposa Spika aruhusu, ijadiliwe.

“Hitaji la vipengele vya 144 na 145 vinavyohusiana na kuondolewa kwa Rais vitatumika katika mchakato wa kumwondoa afisini Naibu Rais,” inasema kipengele cha 150 ibara ya 2.

Hoja hiyo shart ieleze wazi makosa ya Naibu Rais kama vile ukiukaji wa katiba au sheria nyingine, kutenda uhalifu kinyume na sheria za kitaifa au kimataifa na mienendo isiyokubalika.

Mbunge anayedhamini hoja kama hiyo sharti aiandamanishe na ushahidi tosha, ikiwemo hatikiapo, kuthibitisha madai dhidi ya Bw Gachagua.

Spika akiridhika kuwa mahitaji hayo yametimizwa, ataidhinisha kujadiliwa kwa hoja hiyo na kupigiwa kura katika kikao cha bunge lote.

Ikiwa angalau thuluthi mbili ya wabunge, yaani wabunge 233, wataiunga mkono, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula atamjulisha mwenzake wa Seneti Amason Kingi kuhusu uamuzi huo ndani ya siku mbili.

Ndani ya siku saba baada ya Bw Kingi kupokea notisi hiyo kutoka kwa Wetang’ula, ataitisha kikao cha Seneti kusikiza na kujadili shutuma dhidi ya Naibu Rais.

Sawa na utaratibu unaotumika kushughulikia hoja ya kuwatimua magavana, Seneti inaweza kuamua kwamba hoja hiyo ichunguzwe na kamati maalum yenye wanachama 11.

Kamati hiyo itachunguza suala hilo, na kuwasilisha ripoti kwa kikao cha maseneta wote ndani ya siku 10, kubaini ikiwa madai dhidi ya Naibu Rais yamethibitishwa.

Naibu Rais atapewa nafasi ya kufika mbele ya kamati hiyo kujitetea dhidi ya tuhuma hizo au awakilishwe na wakili wake.

Endapo kamati hiyo maalum itaripoti kuwa vipengele katika mojawapo ya shutuma dhidi yake havijafafanuliwa ipasavyo, mchakato huo utakomea hapo.

Kwa upande mwingine, ikiwa kamati hiyo itaripoti kuwa vipengele katika mojawapo ya makosa hayo matatu vimefafanuliwa kwa njia sawa, Naibu Rais atapewa nafasi ya kujitetea kabla ya maseneta kupiga kura.

Ikiwa angalau thuluthi mbili ya maseneta, yaani maseneta 47 kati ya 67, wataidhinisha mojawapo ya mashtaka hayo, Naibu Rais atakuwa ameondolewa afisini.

Lakini hata baada ya maseneta kumwondoa rasmi afisi, Naibu Rais bado anao mwaya wa kupinga hatua hiyo mahakamani.

Ni kwa msingi huo ambapo mchangunuzi wa masuala ya kisiasa Barasa Nyukuri anawashauri wabunge wanaopiga vifua kuwa watamtimua Bw Gachagua kuchunguza upya mkakati huo.

“Ikumbukwe kuwa aliyekuwa Gavana wa Embu Martin Nyaga Wambora aliokolewa na Mahakama na akahudumu kwa miaka 10 licha ya Seneti kumtimua mara mbili,” anasema.

“Ama kwa hakika, hoja ya kumtimua Naibu Rais itakabiliwa na changamoto kubwa hata katika ngazi ya Bunge la Kitaifa na lile la Seneti kwa sababu kupatikana kwa wabunge 233 na maseneta 47 wa kuunga mkono hoja kama hiyo hakutakuwa kazi rahisi. Kuna wengi ambao hawataunga mkono hoja kama hiyo kutokana na sababu nyingi,” Bw Nyukuri akaongeza.