Habari za Kitaifa

Utahitaji Sh600,000 mkononi kupata kazi ya polisi, ripoti ya Maraga yaonyesha

Na ALEX NDEGWA, KAMORE MAINA September 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UFISADI wa hali ya juu katika Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) unaojumuisha hongo katika uajiri na jinsi wakuu wa polisi wanavyoingiza mabilioni ya pesa kupitia rushwa kutoka kwa madereva wa magari umefichuliwa katika ripoti iliyokabidhiwa Rais Ruto, ambayo pia inaelezea mpango wa kisasa wa Sh106 bilioni.

Mbali na imani kwamba sifa na utimamu wa mwili huongoza uajiri wa maafisa wa polisi, ripoti hiyo inafichua kuwa kazi hiyo inauzwa kwa Sh600, 000, huku wale wanaotoa hongo wakiepuka mazoezi makali wakati wa usajili ikiwa ni pamoja na mbio za barabarani.

Ufisadi kama huo unaenea hadi uajiri wa maafisa waliohitimu ambao unafaidi watoto na jamaa wa watu wenye nguvu wakiwemo maafisa wakuu wa polisi, upendeleo unaohakikisha kwamba uongozi wa huduma hiyo uko mikononi mwa walio mamlakani.

Ripoti hiyo inafichua jinsi hongo zinazokusanywa kutoka kwa madereva wa magari na maafisa kutoka Kitengo cha Polisi wa Trafiki zinavyowasilishwa hadi kufikia wakubwa huku ushindani wa hongo ukilaumiwa kwa vizuizi vingi vya barabarani, vingine vikiwekwa karibu sana kutoka kila kimoja.

Biashara ya uhalifu ina faida kubwa sana hivi kwamba ripoti inasema mara nyingi, mkuu wa kituo hutoa gari rasmi la kituo cha polisi, ambalo kawaida huegeshwa kwenye kizuizi cha barabara na hutumika kusaidia katika ukusanyaji wa rushwa badala ya kutekeleza majukumu mengine yanayopaswa kupewa kipaumbele.

Maelezo haya ya kushangaza yamo katika ripoti ya Jopo Kazi la Kitaifa la Uboreshaji wa Sheria na Masharti, na Marekebisho mengine kwa maafisa wa Polisi, Huduma ya Magereza ya Kenya na Huduma ya Vijana kwa Taifa iliyowasilishwa kwa rais mnamo Novemba, 2023.

Jaji mkuu mstaafu David Kenani Maraga aliongoza jopokazi la wanachama 19 ambao ripoti yao kamili haijawahi kutolewa kwa umma lakini Taifa Leo ilipata nakala. Ripoti inapendekeza ununuzi wa vifaa vya kisasa kama vile helikopta na silaha pamoja na kupandishwa kwa mishahara na uboreshaji wa vifaa katika mpango utakaogharimu Sh106 bilioni ili kuimarisha Huduma ya Taifa ya Polisi.

Wiki jana, Rais Ruto alianzisha utekelezaji wa mapendekezo ya jopokazi la Maraga katika mkutano uliofanyika Shule ya Serikali ya Kenya ambapo alitangaza kuwa Sh45 bilioni zimetengwa kwa ununuzi wa vifaa.

Sh22 bilioni nyingine zimetengwa kuboresha mishahara na marupurupu ya maafisa na Sh37 bilioni zitatumika katika uboreshaji wa vifaa zikiwemo nyumba.

Ripoti hiyo inafichua hali ya kusikitisha ya kitengo cha polisi wa angani na ufichuzi kuwa ndege 24 hazitumiki zikiwemo tano ambazo zimewahi kuanguka.

Inafichua mzozo kati ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) na wakuu wa polisi baada ya ndege za polisi kuhamishwa hadi Idara ya Kitaifa ya Anga (NASD), ambayo iko chini ya KDF.