Habari za Kitaifa

Ndoto ya elimu ya juu yaning’inia padogo kwa wanafunzi 50,000 wa vyuo vikuu


TAKRIBAN wanafunzi 50,000 wa mwaka wa kwanza katika vyuo vikuu hawajalipa karo zao hata baada ya kupokea ufadhili kutoka kwa serikali chini ya muundo wa ufadhili wa elimu ya juu na hivyo kuwa katika hatari ya kutofanya mitihani yao mwishoni mwa muhula.

Kutokana na hayo, wabunge Jumanne walimwagiza waziri wa Elimu Julius Ogamba kuagiza vyuo vikuu kuwaruhusu wanafunzi hao kufanya mitihani hata kama hawajalipa karo zao kikamilifu.

Kati ya wanafunzi 138,535 waliotengewa nafasi katikaVyuo Vikuu Kenya, 124,364 tayari wameripoti. Hata hivyo,  75,000 tu kati yao ambao wameweza kulipa karo yao ya masomo kikamilifu.

Taarifa hizo zilijitokeza Bw Ogamba alipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Kitaifa kuhusu Elimu. Wabunge hao walionyesha kusikitishwa na utekelezaji wa muundo wa ufadhili wa elimu ya juu, wakitaka wanafunzi waruhusiwe kufanya mitihani ili wasiathirike serikali inapotatua changamoto zinazokabili mfumo huo.

Wabunge hao walitaka muundo mpya wa ufadhili wa elimu ya vyuo vikuu ufanyiwe marekebisho baada ya karibu nusu ya wanafunzi kuwekwa katika makundi yasiyofaa.

“Tafadhali waziri, andika barua kuelekeza vyuo vikuu viruhusu wanafunzi  kufanya mitihani kabla ya suala hili kushughulikiwa,” mwenyekiti wa kamati hiyo Julius Melly alisema.

Mbunge wa Marakwet Mashariki Timothy Toroitich alipendekeza muundo huo mpya wa ufadhili usitishwe ili kuruhusu Bunge kuuchunguza.

Kulingana na Bw Ogamba, wanafunzi 11,132 wamekata rufaa dhidi ya mgao wa ufadhili wa masomo na mikopo ya wanafunzi. Kati ya hao, wanafunzi 6,548 walitaja gharama kubwa za kozi wanazosoma kuwa changamoto kuu. Wanafunzi hao wamewekwa katika kundi la 4 (2,150) na kundi la 5 (2,433).

Chini ya kundi la  4, wanafunzi hupata ufadhili wa juu wa asilimia 40 ya gharama ya masomo, asilimia 30 kama mkopo na familia inatarajiwa kulipa asilimia 30 iliyobaki na vile vile utunzaji wa mwanafunzi akiwa chuo kikuu.

Wanafunzi katika kundi la 5 wanapata kiwango cha juu cha asilimia 30 ya gharama ya mpango kama ufadhili wa masomo, mkopo wa asilimia 30 na  familia inatarajiwa kugharamia asilimia 40. Gharama ya  masomo katika vyuo vikuu ni kati ya Sh144,000 na Sh600,000.