Majaji wazima tena nyota ya Pasta Ezekiel
MAHAKAMA ya Rufaa imetupilia mbali ombi la Pasta Ezekiel Odero la kutaka agizo la kusitisha kufutiliwa mbali kwa leseni ya kanisa lake lililoko kaunti ya Kilifi, hadi kesi yake itakapomualiwa.
Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa walitupilia mbali ombi hilo wakisema kuwa Pasta Odero alishindwa kutumia utaratibu uliopo wa kutatua migogoro, kabla ya kuwasilisha kesi mahakamani.
Pasta Odero alipinga kufutwa kwa usajili wa Newlife Prayer Center & Church (NPCC) mnamo Mei 18, mwaka jana, kwa kushindwa kuwasilisha ripoti za kila mwaka inavyohitajika kisheria.
Majaji Daniel Musinga, Kathurima M’Inoti na Mwaniki Gachoka walisema kuwa badala ya kukata rufaa kwanza kwa Waziri wa Masuala ya Ndani kufuatia kufutwa kwa leseni ya kanisa lake, Bw Odero aliwasilisha kesi mahakamani.
“Kwa kuzingatia maamuzi thabiti ya mahakama hii na Mahakama ya Juu kwamba ni lazima kwanza mtu atumie taratibu za utatuzi wa migogoro zilizotolewa na sheria kabla ya kukimbia Mahakama Kuu, tumeridhika kuwa rufaa hii haifai. Kwa hivyo, inatupiliwa mbali,” walisema majaji.
Mahakama iliambiwa kwamba NPCC ilishindwa kuwasilisha ripoti yake ya mwaka na Aprili 13, 2023 na Msajili wa Vyama alilitaka kuwasilishwa mwaka ya 2021/2022.
NPCC haikufuata sheria na mnamo Aprili 27, 2023, Msajili alimpa pasta Odero siku 21, kueleza kwa nini usajili haungefutwa.