Sababu ya Kenya kulengwa zaidi na magaidi kuliko mataifa jirani
Na VALENTINE OBARA
LICHA ya mafanikio makubwa ambayo Kenya imepata katika vita dhidi ya ugaidi, nchi hii bado hukodolewa macho na tishio hilo kutokana na sababu mbalimbali.
Kenya ni miongoni mwa nchi zilizo na wanajeshi wake kwenye kikosi cha Wanajeshi wa Muungano wa Afrika walio Somalia (AMISOM), ambao wanashiriki katika vita vya kupambana na magaidi wa kundi la magaidi la al-Shabaab.
Kwa msingi huu, magaidi hao ambao wamezidi kulemewa kivita ndani mwa Somalia, huingia humu nchini kushambulia raia wasiokuwa na silaha zozote.
Mashambulio haya hunuiwa kushinikiza Kenya iondoe wanajeshi wake nchini humo, hatua ambayo Rais Uhuru Kenyatta husisitiza haitachukuliwa hadi kundi hilo liangamizwe kabisa na utulivu kurejea Somalia.
Hata hivyo, maswali huibuka kuhusu kwa nini mashambulio mengi yanatokea Kenya ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika zilizo na wanajeshi katika AMISOM kama vile Uganda na Ethiopia.
Tafiti za mashirika mbalimbali zinazohusu masuala ya kiusalama husema Kenya huwa hatarini zaidi kwa sababu ya jinsi inavyokaribiana sana na Somalia.
Magaidi wamekuwa wakiingia nchini kupitia kaunti za Mandera, Wajir, Garissa na Lamu ambazo zimo kwenye mipaka yenye ulinzi hafifu. Mpango wa serikali kujenga ukuta wa kuimarisha usalama mpakani haujakamilika.
Mwaka uliopita, Umoja wa Mataifa (UN) ulitoa ripoti iliyodai kuwa magaidi huwahonga polisi wa Kenya mpakani kwa hata Sh2,000 ili kuruhusiwa kuingia nchini. Lakini Inspekta Jenerali wa Polisi, Bw Joseph Boinnet alipuuzilia mbali ripoti hiyo na kueleza jinsi maafisa walivyofanikiwa kuzuia mashambulio mengi.
Kenya pia hulengwa na magaidi kutokana na ushirikiano wake mkubwa na mataifa ya Magharibi ambayo hutumia nchi hii kama makao makuu na kiingilio kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki na ya Kati.
Nchi hizo kama vile Amerika na Uingereza pamoja na mashirika makubwa kama vile UN, ambayo hupenda kuweka afisi zao kuu nchini humo, hasa Nairobi.
Vile vile, nchi hii ingali ni kivutio kikubwa cha watalii wanaotoka mataifa ya magharibi.
Magaidi wakati mwingi hutaka kushambulia raia wa kigeni ili wapate nafasi ya kutumia propaganda kujigamba.
Vile vile, inaaminika huwa ni rahisi kwa magaidi kusajili vijana Wakenya katika makundi yao kwa sababu ya jinsi ukosefu wa ajira ulivyokithiri, na imani kwamba makundi fulani ya kijamii au kidini yametengwa na serikali kwa miaka mingi.
Mashirika ya kijamii na kidini katika miaka ya hivi majuzi yamezidisha juhudi za kuhamasisha vijana dhidi ya kujiunga na makundi ya kigaidi.