Korti yamsamehe mwanaume aliyeshikwa akiwa amevaa chupi ya wanawake na sidiria
MAHAKAMA ya Kenol, Kaunti ya Murang’a, imemsamehe mwanaume aliyefikishwa kortini kujibu mashtaka ya kuiba mitungi sita ya maji na blanketi.
Akitoa uamuzi huo Jaji Mkuu Mkazi Sheila Nyaga alisema masaibu ya mshukiwa yalionekana tofauti na yale yaliyowasilishwa kortini.
Kulingana na upande wa mashtaka, mnamo Septemba 12 katika Kaunti Ndogo ya Murang’a Kusini mwendo wa saa tatu asubuhi, mlalamishi alikuta vipipa vyake sita havipo alipokuwa akijiandaa kuenda kuteka maji.
Akiwa amepigwa na butwaa, alipekuapekua ndani ya boma na kugundua blanketi aliyokuwa ametundika kwenye uzio haipo pia.
Korti ilielezwa kuwa mlalamishi alichukua mitungi iliyobaki na kuelekea kuchota maji – akiwa njiani alivutiwa na kitu.
Ripoti inaarifu aliona blanketi na aliposogea karibu, alikumkuta mshtakiwa akiwa amejifunika blanketi chini ya kivuli. Kando yake, kulikuwa na mitungi sita.
Alipiga nduru
Alipiga ukemi na papo hapo mshtakiwa akatoroka kabla ya kukamatwa na watu waliosikia mayowe ya kutaka msaada.
Baada ya kukamatwa, mshtakiwa aligunduliwa alikuwa amevalia nguo za ndani za wanawake – sidiria na chupi.
Tukio hili lilisukuma watu hao kuita maafisa wa polisi ambao walimkamata na kumfikisha kortini.
Mbali na kuiba mitungi na blanketi, mama ya mshukiwa aliambia mahakama kuwa mwana wake amekuwa akisumbuka siku za hivi karibuni.
Mama huyo alikiri kumuombea mtoto wake ili abadilishe tabia baada ya kutoka kwake Kangari, kuenda kuishi na mama na dada yake.
Alikubali mashtaka na kuhukumiwa kutumia kigezo cha ombi la msamaha.
Hakimu alimsamehe almuradi akomeshe tabia ya usumbufu na atafute msaada wa maombi kama hatua hizi zingesaidia kumboreshea maisha.