Makala

Bunge: Endeleeni kutaptap TikTok Kenya, hatutapiga marufuku

Na SAMUEL OWINO September 28th, 2024 2 min read

KAMATI ya bunge imetupilia mbali rufaa ya kupiga marufuku mtandao wa kijamii wa TikTok nchini.

Badala yake bunge linataka tathmini ya mara kwa mara kubaini kama jukwaa hilo linafuata kanuni zinazotakiwa na mamlaka za taifa.

Katika ripoti iliyowasilishwa bungeni, kamati hiyo ya rufaa ya umma ilisema marufuku ya TikTok haikubaliki kwa sababu itaathiri uhuru wa vyombo vya habari na wa kujieleza.

“Kamati hii inatupilia mbali ombi la kupiga marufuku oparesheni ya TikTok kwa sababu itakiuka haki na uhuru nchini,” kamati iliripoti.

“Marufuku ya moja kwa moja ya TikTok itakuwa na athari mbaya sana kwa uvumbuzi na ubunifu miongoni mwa waandaaji wa vipindi vya kidijitali. Marufuku itaathiri vibaya haki ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari, na zote ni haki za kikatiba kwa demokrasia yetu.”

Kamati hiyo ilibaini kuwa nchi inaelekea kukumbatia mfumo thabiti wa uchumi dijitali na iwapo mitandao ya kijamii itadhibitiwa, itaathiri maendeleo ambayo yameshuhudiwa.

“Marufuku ya jukwaa la kijamii itatibua ustawi wa kijamii na kiuchumi na manufaa ya muunganisho wa intaneti nchini unalenga kuimarisha uchumi dijitali,” ripoti ya kamati ilisema kama ilivyotumwa kwa Rais.

Kamati hiyo, inayoongozwa na Mbunge wa Kitui Mashariki, Nimrod Mbai, inasema mitandao yote ya kijamii nchini, ikiwa ni pamoja na TikTok, inafaa kudhibitiwa na utendakazi wao unapaswa kukaguliwa mara kwa mara na mashirika ya serikali.

Maswali ya kimsingi

Lakini licha ya kuondoa marufuku ya TikTok, kamati hiyo iliibua maswali ya kimsingi kuhusu utendakazi wa jukwaa hilo nchini.

Wasiwasi unaangazia usalama wa taifa na uhifadhi na utunzaji wa data, udhibiti wa maudhui na ukiukaji wa miongozo ya jamii, manufaa ya kiuchumi na iwapo kanuni za nchi zinafuatwa.

Kamati hiyo ilikubali kuwa TikTok ni tisho kubwa kwa usalama wa taifa, suala ambalo kwa sasa linazingatiwa na Baraza la Usalama wa Kitaifa.

“Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya TEHAMA na Uchumi wa Dijitali zitashirikiana kuimarisha ulinzi wa watumiaji na usalama wa mtandao kwenye mitandao ya kijamii, ikiwemo TikTok, na kuripoti Bungeni ndani ya miezi minne baada ya kuwasilishwa kwa ripoti hii,” ilisema ripoti hiyo.

Mnamo Machi mwaka huu, Waziri wa Usalama Kithure Kindiki aliiambia kamati hiyo kwamba Baraza la Usalama la Kitaifa lilikuwa limetilia mkazo kupiga marufuku watumishi wa umma kutumia TikTok kulinda data muhimu.

Kadhalika, kamati hiyo ilifichua kuwa mtandao huo  una athari hasi kwa maisha ya vijana kwa sababu hauna vifaa thabiti na za kutosha za kuwahikishia usalama watumiaji wachanga.

Kutokuwepo kwa ofisi za TikTok nchini pia kulitajwa kuwa changamoto kwa sababu watumiaji hawana pa kuwasilisha malalamishi yao.

Ombi hilo liliwasilishwa Bungeni Agosti 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ushauri ya Bridge Connect, Bob Ndolo, ambaye aliwataka wabunge kupiga marufuku kabisa mitandao ya kijamii, akisema inatumika kuendeleza ukatili na maudhui ya ngono, hasa miongoni mwa vijana.