Habari Mseto

Ofisi ya ODM Kakamega yafungwa kwa kushindwa kulipa kodi ya Sh500,000

Na SHABAN MAKOKHA September 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

AFISI ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) mjini Kakamega imefungwa kufuatia malimbikizo ya kodi ya nyumba ya zaidi ya Sh500,000.

Haya yanajiri huku Gavana Fernandes Barasa, ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho katika kaunti hiyo akifungua afisi mpya katika maeneo mbalimbali katika kaunti hiyo.

Ofisi kumi na moja za kaunti ndogo zimepangwa kufunguliwa na kuwekwa fanicha za kisasa na wafanyikazi.

Mnamo Septemba 26, 2024, Bw Barasa alianza shughuli ya kufungua afisi mpya katika kaunti ndogo katika juhudi za kukifanya chama hicho kuwa maarufu zaidi katika eneo hilo.

Alizindua afisi mpya ya chama cha ODM katika soko la Shianda eneo la Mumias Mashariki huku akiendelea kufufua chama hicho na kukifanya kiwe maarufu zaidi katika kaunti.

Bw Barasa alithibitisha kuwa chama hicho kiko imara na kitaendelea kutawala eneo hilo hata baada ya Bw Raila Odinga kuacha siasa za humu nchini ili kuangazia kampeni zake za kuwania kiti cha AUC.

“Tuko pamoja na nyuma ya uongozi wa maafisa wapya walioteuliwa kufuatia matukio ya hivi punde katika chama chetu,” Bw Barasa alisema.

Alisema ili kuimarisha uwepo wa chama hicho katika kaunti ya Kakamega, alikuwa ameandaa kampeni ya uhamasishaji mashinani na ufunguzi wa afisi mpya.

Lakini licha ya Bw Barasa kukariri kuwa chama hicho kiko imara mizozo inayochipuka inatishia kuhatarisha nguvu yake Kakamega.

Chama hicho kinakabiliwa na mgawanyiko mkubwa huku makundi mawili, moja likiongozwa na Bw Barasa na jingine mbunge mwakilishi wa wanawake Elsie Muhanda wakivutana.

Malumbano kati ya aliyekuwa naibu kiongozi wa chama Wycliffe Oparanya na Bw Barasa, hasa katika uendeshaji wa bunge la kaunti pia yanatishia mamlaka ya chama cha upinzani.

Bw Oparanya alijiuzulu wadhifa wa naibu kiongozi wa chama baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Vyama vya Ushirika lakini bado ana wafuasi wengi wa ODM katika kaunti hiyo.

Bw Barasa ameitaka kamati kuu ya usimamizi ya chama hicho kukoma kusimamia masuala ya Bunge la Kaunti ya Kakamega.