Dimba

Wanabunduki wanyamazisha Foxes licha ya kuwapa ‘maradhi ya moyo’ kipindi cha pili

Na GEOFFREY ANENE September 28th, 2024 2 min read

ARSENAL walipata mabao mawili ya kuchelewa wakiliza Leicester City kwa mabao 4-2 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kudumisha rekodi ya kutoshindwa msimu huu wa 2024-2025 mnamo Jumamosi, Septemba 28, 2024.

Vijana wa kocha Mikel Arteta, ambao sasa wako sako kwa bako na mabingwa watetezi Manchester City kwa alama 14, walifurahia kuenda mapumzikoni kifua mbele 2-0 baada ya Gabriel Martinelli na Leandro Trossard kutetemesha nyavu za Leicester dakika ya 20 na 45, mtawalia.

Hata hivyo, James Justin alipunguza mwanya huo kupitia kichwa baada ya kupokea ikabu safi kutoka kwa Facundo Buonanotte dakika ya pili ya kipindi cha pili. Mpira uligusa Kai Havertz kidogo na kumchanganya kipa David Raya ambaye hakuonenakana akiwa katika hali yake nzuri ya kawaida.

Wanabunduki wa Arsenal waliingia tumbojoto baada ya Foxes kusawazisha kupitia shuti kali kutoka kwa beki wa pembeni kulia Justin.

Arteta kisha alipumzisha Martinelli na kujaza nafasi yake na Raheem Sterling na pia kuingiza kinda Ethan Nwaneri katika nafasi ya Thomas Partey ndani ya dakika 16 za mwisho za muda wa kawaida wakati Foxes wakiweka presha na pia kulinda ngome yao vyema.

Kocha Steve Cooper pia aliwaita nguvu-mpya kwa kupumzisha Buonanotte na kujaza nafasi yake na Jordan Ayew dakika ya 85 na kisha kuingiza Bilal El Khannouss na Bobby De Cordova-Reid mahali pa Oliver Skipp na Stephy Mavididi, lakini Arsenal ndio walipata nafasi ya kupumua baada ya Wilfred Ndidi kujifunga dakika ya 94 kutokana na mpira wa Trossard kufuatia kona ya Bukayo Saka.

Mambo yaliharibikia Leicester zaidi dakika chache baada ya mshambulizi Gabriel Jesus kujaza nafasi ya Trossard nao Odsonne Edouard na Abdul Fatawu kuchukua nafasi za Ndidi na Caleb Okoli kambini wa Leicester, mtawalia.

Hiyo ni baada ya Havertz kupachika bao kutokana na mpira wa kuondoshwa langoni kutoka kwa Justin. Goli hilo lilihitaji kuchunguzwa na teknolojia ya video (VAR) kabla ya kukubaliwa.

Arsenal sasa wamevuna ushindi mara sita mfululizo dhidi ya Leicester ligini. Wameendeleza rekodi duni ya Foxes ugani Emirates hadi vichapo 22, sare nne na ushindi mmoja.

Katika matokeo mengine, City ya kocha Pep Guardiola ilitupa uongozi ikikabwa 1-1 na wenyeji Newcastle United, Chelsea walitoka chini bao moja na kuvunjilia mbali rekodi ya kutoshindwa ya Brighton katika ushindi wa 4-2 kupitia mabao ya Cole Palmer ugani Stamford Bridge, naye Dwight McNeil alifungia wenyeji Everton mabao mawili katika kipindi cha pili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Crystal Palace.

Brentford, ambao wamekuwa klabu ya kwanza katika historia ya EPL kupata bao ndani ya dakika ya kwanza katika mechi tatu mfululizo, waligawana alama na West Ham katika sare ya 1-1 nao Fulham wakamaliza rekodi ya wenyeji Nottingham Forest ya kutoshindwa kwa kuwalaza mbele ya mashabiki wao 1-0.

Kufuatia matokeo hayo, City ya Pep Guardiola ilisalia kileleni kwa alama 14, mbele ya Arsenal kwa ubora wa goli moja.

Ratiba ya mechi za raundi ya sita za EPL:

Septemba 28 – Newcastle 1-1 Manchester City (2.30pm),

Chelsea 4-2 Brighton (5.00pm), Brentford 1-1 West Ham

(5.00pm), Everton 2-1 Crystal Palace (5.00pm), Arsenal

4-2 Leicester (5.00pm), Nottingham Forest 0-1 Fulham

(5.00pm), Wolves vs Liverpool (7.30pm); Septemba 29

– Ipswich vs Aston Villa (4.00pm), Manchester United vs

Tottenham (6.30pm); Septemba 30 – Bournemouth vs

Southampton (10.00pm)