Habari za Kitaifa

Wanabiashara wa Nairobi wanaotoka Mlima Kenya wagusa ‘murima’

Na KEVIN CHERUIYOT September 30th, 2024 2 min read

KUNDI moja la watu kutoka jamii ya Kikuyu wanaoishi Nairobi wamemtaka Naibu Rais kukomesha siasa za kutetea eneo la Mlima Kenya wakiziita za ukabila. Wanasema siaza zake zinawaharibia biashara zao.

Wakiongozwa na Diwani Maalum Cecilia Wairimu, walisema hawana pengine wanapoita nyumbani isipokuwa Nairobi na kwamba hawaungi mkono juhudi za Bw Gachagua za kupigania masilahi ya eneo la Mlima Kenya.

“Hatujui kile wanamaanisha wakitaja Mlima Kenya. Hatufai kujumuishwa katika siasa za Mlima Kenya nyakati za uchaguzi na tunaachwa nje nyakati za uteuzi wa watu katika nyadhifa kuu serikalini,” Bi Wairimu akasema.

Watu hao walimtaka Naibu Rais kufanya kazi na Rais William Ruto ili waweze kutekeleza ahadi walizotoa katika manifesto yao.

“Hatutaki kukumbushwa yale yaliyotendeka wakati wa ghasia baada ya uchaguzi wa 2007. Watu wetu waliumia na hivyo hatutaki ukabila hapa. Mlima Kenya haiko hapa na hatutaki kupiganishwa na jamii zingine. Tunamtambua Ruto kama Rais wetu na hatuko tayari kumpiga vita sasa.” Bi Wairimu akasema.

Katibu mpanga ratiba wa kundi hilo Abdalla Karenjo alisema watu kutoka Mlima Kenya wameanzisha biashara sehemu mbalimbali nchini, ambazo zitakuwa salama tu ikiwa nchi imeungana.

“Hatutaki fujo nchini kwa sababu ikitazama kwa makini hatuna ardhi ya kutosha eneo la Kati mwa Kenya, hatuna ardhi ya kutosha kujenga makazi, hiyo ndio maana tumesambaa kote na tumekaribishwa na watu wa makabila mengine,” Bw Karenjo akasema.

Waliwataka wanasiasa ambao wameanza kufanya kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 wakome, badala yake kuwasaidia Wakenya kwa kupunguza gharama ya maisha.

“Inaudhi kuwaona viongozi wetu juu ya magari wakituhimiza kukumbatia siasa za Mlima Kenya. Tunataka kuwaambia kwamba hatutahadaiwa na siasa za Mlima Kenya na hatutamfuata mtu mwingine sasa isipokuwa Rais,” akaeleza Bw Karenjo.

Kundi hilo linasema kuwa Bw Gachagua ‘anayejifanya’ kuwa msemaji wa Mlima Kenya hapendekeze mmoja wao kwa uteuzi katika nyadhifa kuu serikalini.

“Wakati wa uteuzi wa mawaziri na makatibu wa wizara Gachagua hakutoa nafasi yoyote kwa Wakikuyu wa Nairobi. Waliteuwa watu kutoka Murang’a, Kiambu, Nyeri na maeneo mengi. Kwa hivyo, tunakataa kampeni zake,” Francis Mbichi akasema.