HabariHabari za Kitaifa

UDA, ODM zavuna vinono pesa za vyama vya kisiasa

Na VICTOR RABALLA September 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

CHAMA cha UDA chake Rais William Ruto pamoja na kile cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, vimevuna donge nono baada ya kupokea Sh372 milioni zaidi kutoka kwa Hazina ya Vyama vya Kisiasa ikilinganishwa na mwaka uliopita.

UDA ndiyo imepokea kitita kikubwa zaidi – karibu mara mbili ya donge la ODM; chama hicho tawala kimepata Sh558 milioni huku kile cha chungwa kikipokea Sh298 milioni.

Pesa hizo zilisambazwa kwa kutegemea ubabe wa chama katika uchaguzi mkuu wa 2022. UDA ilizoa viti vingi vya ubunge ikivuna wabunge 138 maseneta 22 nayo ODM ikazoa wabunge 86 na maseneta 13.

Kinara wa ODM, Raila Odinga, akihutubia Baraza la Kitaifa la Usimamizi wa Chama (NGC) katika ukumbi wa Bomas, Nairobi, mnamo Aprili 2024. PICHA | WILFRED NYANGARESI

Kupitia notisi katika Gazeti Rasmi la Serikali lililochapishwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu, chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kilipokea Sh130.8 milioni nayo Wiper ambayo nyapara wake ni Kalonzo Musyoka ikatia kibindoni Sh69.8 milioni.

Jubilee ina wabunge 28 na maseneta wanne huku Wiper ikiwa na wabunge 26 na maseneta watatu. DAP-Kenya yake Eugene Wamalwa yenye wabunge watano imepewa Sh30.6 milioni nayo UDM ikazoa Sh26 milioni.

KADU-Asili, Green Party pia zapokea posho

Vyama vingine ambavyo vilikuwa kwenye orodha ya 10-bora katika mgao huo ni ANC ya Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi (Sh25.7 milioni), Ford Kenya ya Spika Moses Wetang’ula (Sh25 milioni), Kanu ya Gideon Moi (Sh23.2 milioni) pamoja na DEP maarufu kama Mbus ya Gavana wa zamani wa Meru Kiraitu Murungi (Sh7.5 milioni).

Kati ya vyama vyote ambavyo vilipokezwa mgao mwaka huu, vilivyopokea kitita kidogo zaidi ni JFPK (Sh268,024), KADU-Asili (Sh464,348) na Green Thinking Action Party of Kenya (Sh563,774).

Kigezo kikuu zaidi kabla ya ugavi wa fedha hizo ni idadi ya kura ambazo kila chama ilipata katika uchaguzi mkuu.