Wezi wamuua mlinzi na kuiba sadaka ya Sh115,000
MAAFISA wa polisi katika eneo la Loitoktok, Kajiado Kusini, wanachunguza kisa ambapo mlinzi wa usiku wa Kanisa la Katoliki aliuawa Jumapili usiku na Sh115,000 zikaibwa.
Genge la majambazi linasemekana kuingia kanisa hilo usiku kupitia ua wa miti kabla ya kumshambulia mmoja wa walinzi waliokuwa wameshika doria.
Kamanda wa Polisi, Loitokitok, David Maina, alieleza Taifa Leo kuwa washambuliaji walimuua mlinzi mmoja lakini mwenzake alifanikiwa kutoroka. Mlinzi wa usiku, 35, aliyeuawa anatoka taifa jirani la Tanzania.
“Majambazi walimkata shingo mlinzi wa usiku kwa kutumia kifaa chenye makali na kumuua papo hapo. Inatatanisha jinsi mwenzake alivyowakwepa wezi hao bila kugundua kifo cha mwenzake hadi nyakati za asubuhi,” alisema Bw Maina.
Shambulizi hilo liliripotiwa na kasisi wa kanisa hilo, Charles Ndemange baada ya kupata mwili wa marehemu ukiwa umelowa damu na kugundua afisi ya kanisa imeibiwa.
Inasemekana wezi hao kisha walielekea kwenye afisi ya kanisa ambapo walivunja mlango na kutoweka na Sh115,000 zilizokusanywa kama sadaka katika ibada ya Jumapili. Hela hizo zilipangiwa kuhifadhiwa kwenye benki Jumatatu.
“Tunashuku njama kutoka ndani. Ni lazima wizi huo ulikuwa umepangwa ikizingatiwa hawakuiba kitu chochote kingine na yamkini walijua mahali hela zilihifadhiwa,” alisema Bw Maina.
Mwili wa mlinzi umehifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Loitokitok.