Habari Mseto

Mount Kenya University yaanzisha kozi ya ubaharia ‘kwa ajili ya ajira za nje’

Na LAWRENCE ONGARO October 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

CHUO Kikuu cha Mount Kenya kimeanzisha kitengo cha kutoka mafunzo ya ubaharia katika chuo cha Malindi Maritime Academy.

Katibu katika Wizara ya Uchimbaji Madini na Uchumi wa Majini Bw Geoffrey Kaituko alipongeza hatua hiyo akisema itachangia kubuniwa kwa nafasi za ajira katika sekta ndogo ya ubaharia.

“Aidha, kuanzishwa kwa kozi hii ya ubaharia kutawatayarisha wanafunzi kupata ajira nje ya nchi,” akasema.

Bw Kaituko alisema hayo alipoongoza hafla ya kutoa hati ya kibali kwa Chuo Kikuu cha Mount Kenya kuanzisha kozi ya ubaharia katika Malindi Maritime Academy.

“Uzinduzi huu ni muhimu sio tu kwa kuienzi Chuo cha Mount Kenya bali utaiweka Kenya kwenye ramani ya ulimwengu haswa katika nyanja ya ubaharia,” akasema.

Bw Kaituko alisema serikali inaendeleza ushirikiano na nchi za Ujerumani, Japan, Korea Kusini na China katika nyanja ya mafunzo ya ubaharia.