Habari Mseto

SHAMBULIO: Wanahabari wa NTV wasimulia hali ilivyokuwa Riverside

January 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

MWANAHABARI wa NTV Silas Apollo na mpiga picha wake Dickson Onyango ni baadhi ya watu ambao wameokolewa kufuatia vamizi la hoteli ya Dusit, eneo la Riverside, Nairobi.

Wanahabari hao waliokolewa takriban saa 12 baada ya uvamizo huo kutekelezwa, baada ya kujificha chooni katika ghorofa ya pili ya jingo pamoja na watu wengine hatari ilipotokea ghafla.

Bw Apollo na Bw Onyango walikuwa wameenda kufanya mahojiano na maafisa wa Tume ya Ugavi wa Rasilimali (CRA) katika ofisi zao za Grosvenor, Riverside, wakati vamizi lilipotokea.

Bw Apollo, katika kikundi moja cha Whatsapp alisema kuwa wakiwa ndani angesikia milio ya risasi katika jingo lote.

“Wamekuwa wakizunguka jingo na kupiga risasi ovyoovyo. Inatisha sana. Niko ndani ya jingo ambalo limevamiwa. Ni kweli. Nilikuwa nimeenda kuhoji watu wa CRA, nahofia maisha yangu sana,” akasema Bw Apollo.

“Kumetulia sasa, japo tunasikia mtu akijaribu kuvunja madirisha. Hatujui wavamizi walipo ama lengo lao,” akaongeza Jumanne saa kumi jioni.

“Tumejaa chooni na watu kadha. Nahofia sana,” mwanahabari huyo akaendelea.

Kwa bahati nzuri, baadaye waliokolewa, pamoja na watu wengine 50 saa kumi alfajiri.

Mwanahabari huyo alisema kuwa walipokuwa ndani, walikuwa wakisonga kwa kutambaa na wengine Zaidi ya 15 hadi walipofika katika ukumbi mkuu wa jingo.

Wanahabari hao walikaa ndani ya jingo kwa zaidi ya saa 15 tangu walipoingia kufanya mahojiano hadi kuokolewa kwao.