Dimba

Mchecheto Arsenal ikialika PSG kwa pambano la UEFA

October 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA wa Arsenal Mikel Arteta anasema timu yake itacheza na timu ya Paris St-Germain (PSG) katika “kiwango cha juu zaidi” watakapomenyana katika Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya ugani Emirates, Jumanne.

Mechi nyingine nane zimeratibiwa kusakatwa leo kote bara Ulaya.

Wanabunduki wa Arsenal watamenyana na PSG ambao ni mabingwa wa Ufaransa baada ya kutoka sare tasa na Atalanta ya Italia katika mchezo wao wa kwanza wa UEFA msimu huu ugenini wiki mbili zilizopita.

PSG nao walipata ushindi wa 1-0 dhidi ya Girona ya Uhispania katika mechi yao ya kwanza na wametinga hatua ya nusu-fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Ulaya katika misimu mitatu mfululizo kati ya mitano iliyopita.

“Upinzani tunaokabiliana nao leo labda ni wa kiwango cha juu zaidi unaoweza kupata katika soka ya bara Ulaya,” alisema Arteta, ambaye aliichezea PSG kati ya mwaka wa 2001 na 2002.

“Lakini ni fursa nzuri kwetu kuona jinsi tunavyokabiliana nao na jinsi tulivyo tayari na namna tunavyoweza kujiweka sawa na kujizolea alama muhimu katika mazingira ya aina hii.”

Arteta pia alisema mabeki Ben White na Riccardo Calafiori wako tayari kuchaguliwa kuunga kikosi cha kwanza katika mechi hiyo.

White amekosa mechi mbili zilizopita za The Gunners kutokana na jeraha la goti huku Calafiori akipona jeraha la mguu wake wa kushoto baada ya kuumia wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyoshuhudia Arsenal wakivuna ushindi wa 4-2 dhidi ya Leicester City ugani Emirates, Jumamosi.

Hata hivyo, PSG watakosa huduma za mchezaji tegemeo Ousmane Dembele ambaye anauguza jeraha la paja.

Katika mechi nyingine zinazotarajiwa kuwa za kusisimua zaidi, mabingwa watetezi wa EPL Manchester City watakabana koo na Slovan Bratislava ya Slovakia ugani Stadion Tehelne pole huku miamba wa Uhispania Barcelona wakialika Young Boys kutoka Uswisi.

AC Milan kutoka Italia watakuwa wageni wa Bayer Leverkusen nchini Ujerumani huku Inter Milan wakipepetana na Red Star Belgrade ya Serbia ugani San Siro, Italia.

Vijana wa Pep Guardiola, Man-City, wako katika nafasi bora ya kushinda baada ya kuanza kampeni zao za UEFA msimu huu kwa sare tasa dhidi ya Inter wiki mbili zilizopita ugani Etihad.

Miamba hao watashuka dimbani siku tatu baada ya kusajili sare ya 1-1 dhidi ya Newcastle United katika EPL. Penalti ya Anthony Gordon wa Newcastle ilifutilia mbali bao la Josko Gvardiol wa Man-City kwenye gozi hilo lililochezewa St James’ Park.