Habari za Kitaifa

Ni kupambana na hali mahakama ikikataa kuzuia mishahara kumegwa kwa ajili ya SHIF

Na SAM KIPLAGAT October 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UTEKELEZAJI wa kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) utaendelea kama ilivyopangwa baada ya Mahakama Kuu Jumanne kukataa ombi la kuisitisha.

Jaji Bahati Mwamuye alikataa kutoa maagizo ya kuzuia wizara ya Afya kutekeleza mpango huo mpya kama ilivyoombwa na Seneta wa Busia Okiya Omtatah, Bw Eliud Karanja Matindi na Dkt Magare Gikenyi.

Watatu hao, walikuwa wamedai kuwa Sheria ya Afya ya Bima ya Kijamii ilikuwa ikitekelezwa bila kupitishwa kwa sheria tanzu zinazoiwezesha.

Hata hivyo, Jaji Mwamuye aliidhinisha ombi hilo kuwa la dharura na kuwaagiza waliowasilisha , Bi Deborah Barasa na Mwanasheria Mkuu, Bi Dorcas Oduor mara moja stakabadhi za kesi.

“Notisi ya kesi imeidhinishwa kuwa ya dharura na itapatiwa kipaumbele kusikilizwa,” alisema jaji. Walalamishi hao watatu pia wametilia shaka ununuzi wa kampuni ya Safaricom ili kutoa Mfumo wa Teknolojia ya Habari ya Afya (IHTS) kwa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC) kwa gharama ya Sh104.8 bilioni.

“Walalamishi wanasisitiza kwamba SHIF haiwezi kutekelezwa bila kuwepo kwa sheria za kuiwezesha chini ya Sheria ya SHA na kuidhinishwa na Bunge,” Bw Omtatah alisema.

Apeiro Limited, yenye hisa nyingi zaidi katika Safaricom ilipatiwazabuni ya kuweka mfumo wa teknolojia wa UHC.

Seneta huyo aliteta kuwa mfumo wa Safaricom na washirika wake unatiliwa shaka kwa vile haukuwa wa uwazi, wenye ushindani na wa gharama nafuu.

Wakenya watakuwa wakichangia asilimia 2.75 ya mapato yao kwa SHA, ambayo inalenga kufanikisha huduma bora na sawa za afya kwa wote.

SHA imechukua nafasi ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF), kwa lengo la kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kupitia nyongeza ya makato ya kila mwezi.

Waziri wa Afya alithibitisha kwamba kufikia Jumatatu Wakenya wasiopungua 2.16 milioni walikuwa wamejiandikisha kwa SHA kabla uzinduzi rasmi.

Wizara ya Afya inalenga kukusanya Sh148 bilioni kuboresha mfumo wa afya nchini katika azma ya kuhudumia afya kwa wote, hasa wale wasio na uwezo.

Utekelezaji wa SHIF unaanza huku kaunti 17 zikikosa wataalamu wa magonjwa ambayo hazina inalenga kushughulikia kamaa afya ya akili, na kuwanyima maelfu ya wagonjwa matibabu wanayohitaji sana.

Kaunti hizo 17 ni pamoja na Kaunti ya Tana River, Lamu, Taita Taveta, Garissa, Marsabit, Isiolo, Nyandarua, Kirinyaga, Turkana, Samburu, Uasin Gishu, Nandi, Narok, Busia, Homa Bay, Migori na Nyamira.

Dkt Chitayi Murabula, Rais wa Chama cha Madaktari wa Akili nchini Kenya, anafichua kuwa kaunti nyingine zina daktari mmoja au wawili wa magonjwa ya akili wanaohudumia zaidi ya watu milioni 1.3.