Makala

Serikali kuvamia Mpesa na ‘airtime’ za wakopaji kujilipa deni la Hasla Fund

Na SAMWEL OWINO, BENSON MATHEKA October 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

AKAUNTI za M-Pesa za watu milioni 13 wanaokataa kulipa mkopo wa Hazina ya Hasla zitavamiwa na serikali ili kurejesha jumula ya Sh7 bilioni.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Hustler Fund Elizabeth Nkukuu aliambia kamati ya Bunge kuwa, kwa sasa wanazungumza na kampuni za simu kuhusu jinsi ya kutelekeza mchakato huo ili serikali irejeshe kiasi hicho kikubwa cha fedha.

Akiwa mbele ya kamati ya Bunge la Kitaifa, Bi Nkukuu aliwaambia wabunge kwamba, wengi wa waliochelea kulipa mikopo ni wale waliokopa katika miezi miwili ya kwanza hazina hiyo ilipozinduliwa.

“Haya ni mazungumzo bado yanaendelea na kampuni za simu kukata pesa hizo kutoka kwa na M-Pesa na ada za mazungumzo,” Bi Nkukuu aliambia kamati.

Kufikia sasa takriban Wakenya 24 milioni wamekopa Sh57.8 bilioni kutoka kwa hazina hiyo, huku watu milioni mbili kwa sasa wakiwa katika hali nzuri kwa kulipa mkopo.

Wakati huo huo, wakulima wa kahawa wamejaa matumaini licha ya changamoto tele, huku mabadiliko yaliyoanzishwa na serikali yakitarajiwa kuzaa matunda zaidi.

Wakulima wa kahawa walipata Sh24.3 bilioni kutokana na mauzo ya magunia 691,956 katika Soko la Kahawa la Nairobi (NCE) katika msimu wa 2023/2024, uliokamilika mwishoni mwa wiki jana.

Ni mwaka ambao ulishuhudia ukosefu wa uaminifu kati ya wakulima na wahusika katika sekta hiyo kufuatia kucheleweshwa kwa utumaji pesa katika akaunti za benki za vyama vya ushirika na changamoto zingine.

Kati ya Oktoba na Desemba, Naibu Rais Rigathi Gachagua aliwasihi wakulima wa kahawa kuuza kahawa yao kupitia NCE, baada ya wengi kukataa kufanya hivyo huku wakitaka kuendelea kufanya biashara na wafanyabiashara wa zamani.

Mnamo Januari, mabroka wa kahawa wakiongozwa na Kirinyaga Slopes, Alliance Berries na New KPCU, walishawishi vyama vya ushirika kupeleka kahawa yao ili iuzwe kwa mnada.

Katika mwaka uliopita, uzalishaji wa kahawa, kulingana na Mamlaka ya Chakula na Kilimo (AFA), ulikuwa ni tani 32,652 kupitia mnada, na tani 9,350 kupitia mauzo ya moja kwa moja.

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa NCE, Lisper Ndung’u, katika mwaka huo, walifanikiwa kuuza mnadani magunia 691,956 ya kahawa na wako na matumaini kuwa mwaka ujao idadi hiyo itaongezeka.

Ndung’u alisema mahitaji ya kahawa bora yamekuwa makubwa na akawataka wakulima kuongeza uzalishaji.

Naibu Rais Rigathi Gachagua, wiki jana alihakikisha wakulima wa Kahawa kwamba mabadiliko anayosimamia yanazaa matunda kauli ambayo Ndungu anakubaliana nayo.

“Mashirika ya udhibiti yamekuwa yakifanya kila yawezalo kuhakikisha utekelezaji kamili wa udhibiti na kuboresha mapato ya wakulima katika soko la mnada,” alisema Ndung’u.

Katika mwaka huo, Alliance Berries iliuza magunia 189,845 ya kahawa ambayo yalizoa Sh6.8 bilioni, New KPCU iliuza magunia 145,733 kwa Sh4.8 bilioni na Kirinyaga Slopes iliuza magunia 118,964,06 kwa Sh4.6 bilioni.