Habari za Kitaifa

Wagonjwa waumia bima mpya ya SHIF ikifeli katika hospitali nyingi

Na BENSON MATHEKA, LEON LIDIGU October 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAGONJWA waliokuwa wakitegemea Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF) waliendelea kutatizika huku mpango mpya wa Afya ya Huduma ya Jamii (SHIF) ukifeli hata serikali iliposisitiza kila Mkenya anafaa kujisajili.

Serikali ilisitisha NHIF mwishoni mwa mwezi jana na kuwataka Wakenya kuhamia SHIF.

Hata hivyo, hospitali zilikataa kuhudumia wagonjwa waliohitaji huduma muhimu wanaotegemea bima ya taifa ya afya.

Wakenya walielezea wasiwasi wa wagonjwa wao kufariki baada ya hospitali kukataa kuwahudumia chini ya SHIF na kuwataka walipe pesa taslimu ambazo hawakuwa nazo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) inayotekeleza SHIF, Bw Elijah Wachira alilazimika kuwaomba Wakenya msamaha baada ya mpango huo kuacha maelfu ya wagonjwa kote nchini wakiteseka.

Akiwahutubia magavana kutoka kaunti mbalimbali mjini Naivasha Jumatano wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Baraza la Magavana (CoG) Muthomi Njuki, Bw Wachira alikiri kwamba mfumo wa tekinolojia wa SHIF ulikwama.

“ICT huwa inakosa kufanya kazi wakati unapohiitaji zaidi. Nimewahi kwenda kutoa hotuba na projekta ikaamua kutofanya kazi,” aliwaambia magavana.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mtendaji alisema mfumo huo haukukwama wakati wa usajili bali pia kwa ulifeli kutambua wagonjwa walioenda hospitalini kwa huduma za matibabu.

“Jumanne, tulianza kuzindua SHIF na kuwataka Wakenya wajiandikishe, mchakato ambao ningesema ulifanikiwa hadi asilimia 80.

Kwa nini sisemi asilimia 100? Ni kwa sababu ilionekana wazi kuwa watu wengi walipojaribu kuingia kwenye mfumo, mfumo ulikwama na baadhi ya usajili haukufanikiwa,” aliongeza.

Kulingana na Bw Wachira, walipogundua kilichokuwa kikitendeka, walizungumza mara moja na maafisa wa kiufundi wanaohusika.

“Tuliweza kuhamisha takriban Wakenya 9 milioni kutoka kwa mfumo wa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF),” alifichua.

Jumatano, waliokuwa wanachama wa NHIF walitumiwa ujumbe na SHA kuwajulisha wamehamishiwa SHIF.

Hii ni baada ya idadi ndogo ya Wakenya kujitolea kujisajili kwa mpango huo mpya ambao serikali imekuwa ikipigia debe.

Bw Wachira alikiri kwamba mfumo wa kushughulikia madai haukuweza kufanya kazi kama ilivyodhaniwa kumaanisha kwamba haukuwa ukifanya kazi.

“Tulikuwa na wagonjwa wa kusafisha figo, wagonjwa ambao walihitaji matibabu ya saratani na akina mama wajawazito ambao walihitaji uangalizi wa haraka na kwa hivyo nilichofanya mara moja ni kuandika kutoka Kakamega ambako nilikuwa, na kuahidi hospitali za kibinafsi na za umma kwamba serikali na SHIF italipa madai hayo yote kwa sababu hatutaketi na kutazama Wakenya wakifa,” alisema.

“Bila shaka kuna kile ninachoweza kufanya kwa mtazamo wa sera na ninachoweza kupeleka kwa wakubwa, niliipeleka kwa bodi ya SHA, wizara ya afya pamoja na mkuu wa utumishi wa umma,” Bw Wachira aliambia magavana akiongeza kulikuwa na mkutano kuhusu suala hilo.

Dkt Bill Muriuki, kutoka chama cha Madaktari na Wataalamu wa Meno Kenya (KMPDU), alisema kuwa kuanzishwa kwa SHIF kumekabiliwa na changamoto kubwa kutokana na ukosefu wa ufafanuzi katika muundo na utekelezaji wake.

“Moja ya masuala muhimu zaidi ni kutokuwepo kwa mikataba inayoeleweka kati ya SHIF na vituo vya afya kwani wasimamizi wengi ambao ni wanachama wetu wameibua wasiwasi kuhusu nani atawalipa, ikizingatiwa kuwa SHA bado haijatambua rasmi au kuingia mkataba na hospitali zao. Kutokuwa na uhakika kumetatiza utoaji wa huduma za afya, hasa katika ngazi za huduma za msingi, kutoka zahanati hadi hospitali za Level 5.”

Beatrice Kairu, mtaalamu wa afya wa Kenya alisema mabadiliko hadi SHIF yalifanywa vibaya na uratibu umekuwa duni.