Nahofia maisha yangu, asema Gavana Nassir akiandikisha taarifa kuhusu bloga aliyebakwa
GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, ameandikisha taarifa kwa polisi kuhusu kisa ambapo mwanablogu ambaye alimkosoa kwenye mtandao wa TikTok alitekwa nyara na kulawitiwa.
Gavana, mama yake na baadhi ya maafisa wa kaunti hiyo walikuwa wamehusishwa na kisa hicho ambacho hadi sasa kimesababisha kukamatwa kwa washukiwa wanne.
Akizungumza baada ya kuandikisha taarifa hiyo katika makao makuu ya polisi Mombasa, Bw Nassir aliitaka Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) iharakishe uchunguzi wao ili kuhakikisha haki inatendeka.
“Hii hainihusu mimi, bali kijana ambaye ni mwathiriwa na lazima tufikie mwisho wa hili jambo,” alisema. Alionyesha nia yake ya kumwasilisha mama yake kwa wapelelezi ikiwa hilo litahitajika, akisisitiza hakuna aliye na mamlaka kuliko sheria.
“Nimejitokeza baada ya kuitwa, naomba yeyote mwenye taarifa asaidie katika kutenda haki. Hakuna mtu wa kawaida anayeweza kusema kilichofanyika kilikuwa sawa. Nimezungumza kama mtu aliyekasirishwa na nimeandika taarifa yangu. Walio na habari wanaweza kushirikiana na DCI,” akasema.
Mnamo Jumapili, Waziri wa Ardhi katika kaunti hiyo, Bw Mohamed Hussein, alikamatwa kuhusiana na kisa hicho.
Hata hivyo, aliachiliwa Jumatatu baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kukosa kumshtaki kwa vile kulikuwa na amri inayozuia kukamatwa kwake.
Mnamo Jumatano, Bw Mohamed almaarufu Amadoh, alisema kwamba yuko tayari kusaidia polisi katika uchunguzi kuhusu madai ya unyanyasaji wa mtandaoni yanayohusishwa na kutekwa nyara na kumbaka mwanablogu huyo.
Hata hivyo, Bw Hussein amelilia mahakama kuwa anahofia maisha yake kutokana na vitisho ambavyo amepata kutoka kwa watu wanaodai kuwa maafisa wa DCI.
Bw Hussein alidai katika stakabadhi zake za mahakama kuwa amepokea mawasiliano mbalimbali, moja kwa moja na kwa njia nyingine, ya kumtisha na kumtishia kukamatwa kati ya Septemba 16 na 20.
“Ninahofia maisha yangu. Ni kwa sababu hii ndipo nimefika mbele ya mahakama hii kuomba ulinzi kupitia dhamana ya kunizuia kukamatwa na kuzuiliwa kinyume cha sheria na DCI,” akasema.
Alitaja matukio ya hivi karibuni nchini ambapo watu wanatekwa nyara na kupotea bila kujulikana walipo kuwa ni sababu za kuomba ulinzi kutoka kwa mahakama.
Pia, alilalamika kwamba amekuwa akitishwa kwa sababu ya wadhifa wake, msimamo wake wa kisiasa, na ukaribu wake na Gavana Nassir.
DCI, kupitia kwa Inspekta wa polisi Capius Otieno, ilifichua kwamba Bw Hussein aliitwa kituoni kuhusiana na uchunguzi unaoendelea kuhusu kosa la Unyanyasaji wa Mtandaoni, kinyume na Kifungu cha 27 cha Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandao nambari 5 ya 2018.