Wanarika wanavyounganishwa na nafasi za ajira na kujikuza
KAMPUNI ya Wave 360 Africa imezindua mpango wa kikuza vipaji vya wanafunzi wa vyuo vikuu na kuwaunganisha na mashirika ya kuajiri.
Kampuni hiyo pia inatoa mafunzo kwa wanavyuo kuhusu umuhimu wa ‘kujiuza’ na kujenga uhusiano mwanafunzi anapokuwa shuleni ili akihitimu mchakato wa kutafuta ajira usiwe mzigo.
Zaidi ya 6000 kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali nchini walikutana katika Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta University of Agriculture and Technology (JKUAT) kushiriki katika mpango wa kukuza vipaji na kuwaunganisha na mashirika mbalimbali.
Kwa utaalamu wa mikakati ya masoko ya “Below the Line” (BTL) na “Above the Line” (ATL), kampuni ya Wave 360 Africa inalenga kuunda mazingira jumuishi ya kibiashara yanayonuia kuleta uhusiano halisi na kuweka maslahi ya wanafunzi mbele.
Katika mahojiano, Mkurugenzi Mtendaji wa Wave 360 Africa, Zedekiah Mukoya, alisisitiza kujitolea kwa kampuni hiyo katika kubuni, kuwasilisha, na kuendeleza mikakati inayowahamasisha na kuunda uzoefu wa kudumu miongoni mwa wanavyuo.
“Malengo yetu ni kujenga uhusiano wa kibiashara, kujenga vipaji, kuunda kizazi cha vijana kinachoweza kujitegemea, na kuongeza uelewa miongoni mwao. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, tumeweza kutembelea vyuo zaidi ya 30 na taasisi za TVET, tukiwafikia wanafunzi zaidi ya 100,000,” alisema Mukoya.
Pia alitoa wito kwa sekta binafsi na ya umma kuiga mfano wa Wave 360, unaolenga kuwapa vijana fursa za kujiinua hasa wa vyuo kupitia maonyesho ya talanta na biashara.
“Mbinu hii inaweza kuchochea uvumbuzi wa kisanii na kuleta suluhu ya kudumu kani vijana wetu wataweza kujitegemea,” akaongeza Bw Mukoya.