Habari Mseto

Ikiwa kuna mtu anatumia data yako bila ruhusa, njoo uripoti kwetu – Kassait

Na GEORGE ODIWUOR  October 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

AFISI ya Kamishna wa Kulinda Data ameelezea wasiwasi kuhusu mienendo ya baadhi ya watu kusambaza data za kibinafsi za Wakenya kwa watu wasiowajua bila idhini yao.

Asasi hiyo ilisema kuwa hatua hiyo imechangia ongezeko la visa matumizi ya data hizo za kibinafsi katika utekelezaji wa uhalifu.

Hii ndio maana Kamishna wa Asasi hiyo ya Kulinda Data Immaculate Kassait amewaonya Wakenya dhidi ya kupeana data zao kwa mtu au watu wasiowaamini.

Uhalifu ya unaotekelezwa kwa njia ya mitandaoni ni mojawapo ya changamoto ambazo serikali inapambana nazo wakati huu, Katibu wa Wizara ya Usalama Raymond Omollo amewahi kusema.

Alisema idadi ya waathiriwa inaongezeka kila uchao huku mbinu za kuendeleza uhalifu huo zikiimarika kila wakati.

Kwa mfano, nyakati hizi Wakenya hupigiwa simu au kutumiwa jumbe na watu wasiowajua wakiwataka wawatumie maelezo yao ya kibinafsi.

Aidha, visa vya udukuzi vimeongezeka katika siku za hivi karibuni huku baadhi ya wahalifu wakiiba pesa kutoka akaunti za benki.

Visa vya kudukuliwa kwa akaunti za mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp na Facebook, vya watu fulani vimeongezeka.

Wahalifu hupata maelezo ya kibinafsi ya watu fulani na kuzitumia kuendeleza uhalifu.

Wahalifu wengine pia huiba data kutoka kwa anwani za barua pepe.

Bi Kassait sasa anasema hali hiyo huwezeshwa na watu ambao husambaza data za kibinafsi za watu au maelezo yanayowatambua.

“Tunataka kuongeza ufahamu kuhusu Ulinzi wa Data. Watu wanapaswa kuelewa kuwa data zao zinapasa kulindwa,” akaeleza.

Bi Kassait alisema hayo mjini Homa Bay mwishoni mwa wiki alipoongoza maafisa wa afisi yake kuzindua kampeni ya kutoa uhamasisho kuhusu umuhimu wa kulinda data.

Kampeni hiyo kwa jina, “Data Yako Jukumu lako” inalenga kuwahimiza raia kulinda data zao za kibinafsi.

“Tunataka wananchi kutufikia ikiwa wamebaini kuwa data zao za kibinafsi zinatumiwa vibaya. Kesi hizo zote zinapasa kuripotiwa kwetu,” Bi Kassait akasema.