Kauli ya Ruto kutodhibiti makanisa inavyokinzana na vifo vya Shakahola
RAIS William Ruto amesema serikali haina mpango wa kudhibiti shughuli za kidini nchini.
Kauli yake inafungamana na mjadala mkali kuhusu Mswada wa Kidini (2024) uliowasilishwa katika Bunge la Seneti na Seneta wa Tana River Danson Mungatana.
Mswada huo unapendekeza kuanzishwa kwa afisi ya msajili wa madhehebu ya kidini kama vile makanisa ambayo itakuwa na mamlaka ya kusajili na kufutilia mbali mashirika na viongozi wa kidini wakati wowote.
Mswada huo uliwasilishwa kufuatia mauaji ya Shakahola ambayo yalitikisa nchi, ambapo zaidi ya miili 420 ilichimbuliwa kutoka makaburi kati ya Aprili 25 na Oktoba 2023.
Akizungumza katika kanisa la AIC Milimani mnamo Jumapili, Rais alisema afadhali serikali ifuate Katiba ambayo inatambua uhuru wa kuabudu kuliko kurekebisha sheria.
“Utangulizi wa Katiba ya Kenya unasema ‘Mungu wa wote,’ kumaanisha kuwa sisi sote tuko chini ya Mungu, na ndiyo sababu Kenya itaendelea kuwa taifa linalomcha Mungu. Tutalinda uhuru wa kuabudu katika jamhuri yetu,” Rais akasema.
“Ninajua kuna mapendekezo ambayo yamewasilishwa kudhibiti kanisa. Ninawakumbusha wale ambao wanafuatilia hili kuwa Katiba ya Kenya iko wazi kuhusu uhuru wa kuabudu, na hakutakuwa na udhibiti wowote kwa uhuru wa kuabudu nchini Kenya,” akaongeza.
Rais aliwarai viongozi wa kidini waunde mipango ya jinsi wanapenda usimamizi wa shughuli za kidini uendelezwe bila kuingiliwa na serikali.
Alisema: “Shirika la kidini nchini litaamua njia ambayo wanataka kuhakikisha uhuru wa kuabudu unalindwa,”
Sehemu ya mswada huo tata unapendekeza faini ya Sh5 milioni ama kifungo cha miaka mitatu kwa makanisa ama viongozi ambao hawajasajiliwa; iwapo sheria hiyo itapitishwa bungeni.
Kulingana na mswada huo, mashirika ya kidini yatahitajika kuunda akaunti tofauti za benki kwa ajili ya sadaka na nyingine ya mapato yanayotokana na shughuli nyingine za kibiashara.
“Sadaka, fungu la kumi, michango na zawadi zinazotolewa kwa mashirika ya kidini na taasisi tanzu hazitatozwa ushuru ikiwa shirika litaonyesha kuwa mapato hayo ni kwa madhumuni ya manufaa kwa jamii,” sehemu ya mswada huo inasema.
Kadhalika, mswada huo unazuia mtu yeyote kuanzisha, kusaidia kuanzisha ama kuendeleza shirika la kidini bila kusajiliwa.
Rais hakuongea kuhusu mswada wa kutimuliwa kwa Gachagua ambao umeongeza joto la kisiasa nchini.
Rais Ruto aliliomba kanisa kuombea nchi na kutoa wito wa umoja huku hali ya kisiasa ikiendelea kuwa ngumu nchini.
Hoja ya kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua inatarajiwa kujadiliwa katika Bunge la Kitaifa Jumanne Oktoba 8, 2024.