Habari za Kitaifa

Walimu watishia kususia usahihishaji wa mitihani

Na GEORGE MUNENE October 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MUUNGANO wa Walimu wa Sekondari (KUPPET) umetishia kuwaongoza walimu kususia usahihishaji na usimamizi wa mitihani ya kitaifa kuhusiana na marupurupu duni.

Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori, alisema muungano huo unaitisha malipo ya hadi Sh4,000 kwa siku pamoja na malazi bora kwa walimu wanaosahihisha mitihani ya kitaifa.

Kwa sasa, Baraza la Kiaifa la Mitihani (KNEC) huwalipa watahini, waangalizi na wasimamizi wa vituo vya mitihani Sh400, Sh450 na Sh500, mtawalia kila siku. Muungano huo unasema wasahihishaji wa mitihani hulipwa hadi Sh150 na kupewa makazi duni.

“Hata vibarua katika vituo vya ujenzi wanalipwa malipo bora zaidi kuliko walimu wanaosimamia mitihani ya kitaifa yenye thamani kuu. Hii haikubaliki,” alisema Bw Misori.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Walimu Duniani katika Kaunti ya Embu Jumamosi, Bw Misori alitaka marupurupu hayo yaongezwe kabla ya mitihani kuanza.

Haya yanajiri huku KNEC ikianzisha sheria kali za kuzuia udanganyifu kwenye mitihani ikiwemo kuwabadilisha wasimamizi na kupiga marufuku matumizi ya simu baina ya waangalizi.

Bw Misori ameonya ikiwa KNEC haitatoa jibu mwafaka, walimu watajiepusha na usimamizi wa mitihani.

KNEC inapaswa kujifahamisha kuhusu mikondo iliyopo sasa kiuchumi. “Walimu ni wataalam ilhali wanachukuliwa kama wafanyakazi wasio na ujuzi,” alisema.

Alisema, “Walimu wakuu ambao wana digrii huamka saa kumi unusu alfajiri kwenda kuchukua karatasi za mitihani na wanalipwa Sh500 kwa siku. Manaibu wao hata hawalipwi chochote. Hatutaruhusu hali hii kuendelea,” alisema. Bw Misori alisema Kuppet imepania kuhakikisha malipo bora kwa walimu wanaosimamia mitihani.

Aidha, Bw Misori alielezea hofu yake kuhusu sera za serikali zinazodunisha maslahi na hadhi ya walimu katika jamii.

“Sera hizo duni zinajumuisha kupunguza bajeti za elimu zinazoathiri ajira ya walimu wapya, kuwapandisha vyeo walimu, na ustawishaji wa miundomsingi.”

Alilalamika kuwa ajira ya walimu inazidi kuingiliwa huku walimu wanaostahili wakifungiwa nje.

“Kupendelea jamaa wa familia na ubaguzi ni kawaida katika ajira ya walimu,” alisema.