SHAMBULIO: Historia ya kikosi cha Recce
Na LEONARD ONYANGO
Pendekezo la kuunda kikosi maalumu cha Recce katika kitengo cha GSU lilianza kutolewa na aliyekuwa Waziri wa Kilimo,Bruce Mckenzie mnamo 1964 wakati wa serikali ya Mzee Jomo Kenyatta.
Kikosi cha kwanza cha maafisa 37 wa Recce wa kulinda Mzee Kenyatta kiliundwa mnamo 1965. Maafisa hao wote walikuwa wakitoka jamii ya Wakikuyu.
Mnamo 1966, serikali ya Uingereza ilimtaka Mzee Kenyatta kuongeza maafisa 20 wa Recce kutoka jamii nyinginezo ilmradi wawe waaminifu kwake. Na sasa, sasa kikosi cha Recce kimekita kambi katika eneo la Ruiru na kwa kawaida hutumia bunduki aina ya M16 ambazo hutengenezewa nchini Amerika.
Kikosi hiki maalumu hutumwa kusaidia vikosi vingine vya polisi wa GSU.
Hutekeleza majukumu yanayohitaji uangalifu mkubwa kama vile uokoaji wa watu waliotekwa na magaidi kama ilivyoshuhudiwa katika Jumba la Maduka la Westgate (2013), Chuo Kikuu cha Garissa (2015) na shambulio la Jumatatu katika hoteli ya Dusit D2, Nairobi.
Hupewa mafunzo ya hali ya juu na kikosi hicho kinakadiriwa kuwa na jumla ya maafisa 500.
Maafisa hao huanza kwa kupewa mafunzo ya kawaida katika chuo cha mafunzo cha Embakasi.
Miongoni mwa mambo wanayofundishwa ni kutegua vilipuzi, usalama wa ndani ya majengo, kukabiliana na magaidi, kukabiliana na watekaji nyara wa ndege na uokoaji.
Recce hupata mafunzo ya ziada nchini Israeli, Amerika, chuoni Ruiru, katika eneo la Solio Ranch na kambi ya mafunzo ya Magadi.
Baada ya mafunzo, maafisa wa Recce hugawanywa katika makundi matatu kulingana na eneo walilofuzu. Kikosi cha kwanza ni kile cha kukabiliana na watekaji nyara wa ndege na ugaidi.
Kikosi kingine ni kile cha kukabiliana na mikasa huwa tayari kusaidia polisi wa kawaida wanapolemewa.
Kikosi cha mwisho ni kile cha kulinda watu mashuhuri na hupata mafunzo nchini Israeli na Amerika. Kikosi hiki ndicho kilihusika pakubwa katika kutoa ulinzi kwa kiongozi wa Amerika Barack Obama alipozuru Kenya mnamo 2015.
Recce huvalia ‘kikoti’ chenye mifuko ya kubebea magazini za risasi na huunganishwa na jaketi ya kuzuia risasi kupenya.