Habari za Kitaifa

Wandani wa Gachagua wasimama naye licha ya dhoruba kali Bungeni

Na MARY WANGARI October 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WABUNGE washirika wa Naibu Rais Rigathi Gachagua walijitenga na juhudi za kumtimua hoja hiyo ilipojadiliwa bungeni jana Jumanne.

Wabunge Muthoni wa Muchomba (Githunguri) Mary wa Maua (Maragua) Makali Mulu (Kitui ya Kati) Mwakilishi Mwanamke Njeri Maina ni miongoni mwa viongozi ambapo hawakuchelea kumuunga mkono Bw Gachagua.

Bw Mulu, aliyekuwa wa kwanza kutofautiana na hoja ya kumfurusha Naibu Rais aliwarai wabunge wenzake kuweka kando maslahi ya kibinafsi na kushughulikia masuala yanayowahusu wakenya.

“Nimesikiza mashtaka katika hoja hii na kujiuliza ikiwa yametimiza kiwango kinachohitajika kumuondoa ofisini Naibu Rais,” alisema Bw Mulu.

“Kuhusu hisa, sisi sote ni wanasiasa, tuache unafiki, ni wangapi tunapigania maslahi ya watu wetu?”Alisema.

“Watu wa Kitui Kati wamesema kufa dereva, kufa makanga, kufa mekanika, ninapinga hoja hii. Wakenya wana masuala mazito zaidi ya kukabiliana nayo.”

Kwa upande wake, Mary wa Maua aliwahimiza wafuasi wa Bw Gachagua kuwa na subira akilinganisha matukio ya sasa na kujipiga kifua kwa Azimio baada ya kushindwa katika chaguzi 2022.