Habari Mseto

SHAMBULIO: Wakenya waonyesha umoja baada ya uvamizi

January 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

WAKENYA Jumatano waliendelea kusisimua ulimwengu kwa uzalendo, ukarimu na ushujaa wao kufuatia shambulio la hoteli ya Dusit, Nairobi mnamo Jumanne, baada ya kuungana na waathiriwa wa mkasa huo kwa kutoa mchango wa vyakula, damu na maelezo kuhusu waliko waathiriwa.

Kabla ya giza kuondoka alfajiri ya jana, tayari vikundi mbalimbali, vikiongozwa na mama mmoja ambaye picha yake ilisambaa mitandaoni vilikuwa vimefika eneo la Riverside na kiamsha kinywa na kuwapa maafisa wa usalama ambao usiku kucha walikuwa wakipambana na wauaji hao, kuhakikishia nchi usalama.

Wakenya wengine walijitokeza katika hospitali mbalimbali kutoa damu ili iwafae walioumia katika shambulio hilo. Kwa mfano ,katika kaunti ya Mombasa, wenyeji walijitokeza kwa wingi katika jumba la Koblenz na kupiga foleni ili kutoa damu.

JIjini Nairobi, kampuni ya magari ya usafiri ya teksi, Uber ilijitolea kutoa usafiri wa bure kwa yeyote angetaka kutoa damu, na kuwasafirisha wahisani hadi hospitali za MP Shah na Kenyatta.

Waandishi wa habari, ambao pia wenzao walijipata kwenye njiapanda walitumia mtandao wa Whatsapp kuchangisha fedha na kuwapelekea wanahabari wenzao pamoja na familia zilizokuwa zikisubiri wapendwa wao. Bi Patience Nyange ambaye aliongoza zoezi hilo alisema walifanikiwa kuwanunulia wanahabari wenzao waliokuwa kazini usiku wa baridi vyakula, dawa, na mahitaji mengine ya kimsingi.

“Baada ya kuzungumza kupitia Whatsapp, tulichanga zaidi ya Sh30,000 ambazo tumetumia kununua vyakula, vinywaji na hata dawa na vingine tukawapa maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu kuwagawia watu. Tunatumai kuendelea hadi usiku wa leo kwa kuwa bado kuna watu ambao watakuwa kazini eneo hilo,” akasema Bi Nyange.

Mitandaoni , Wakenya walikuwa wakiimba wimbo wa umoja na kudhihirisha ushupavu wa Kenya, wakianzisha hashitegi za kusifu vikosi vya kiusalama kwa kazi nzuri.

Baadhi ya hashitegi zilizotamba kwenye mtandao wa Twitter ni “#WeShallOvercome, #KenyaUnbowed na #WeAreOne”

Kwingineko, Wakenya walikashifu shirika la habari la Kimarekani, New York Times, kwa kuchapisha picha za waathriwa wa shambulio hilo hadi shirika hilo likaomba msamaha.

Wakenya walilitaka kuwa na maadili na kutochapisha aina za habari ambazo zinakweza magaidi hao.