Habari Mseto

EACC yataka maafisa watano wa utawala wa Ngilu wakamatwe kuhusu ufisadi katika Kicotec

Na COLLINS OMULO, BENSON MATHEKA October 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imetaka maafisa watano wa zamani wa Kaunti ya Kitui washtakiwe kwa makosa ya ununuzi na matumizi mabaya ya fedha kuhusiana na Kampuni ya Nguo ya Kaunti ya Kitui (Kicotec).

Haya yanajiri huku kamati ya Seneti ikitangaza kampuni hiyo kuwa eneo la uhalifu na kuibua wasiwasi kuhusu shughuli za kutiliwa shaka wakati wa utawala wa aliyekuwa Gavana Charity Ngilu.

Wakiwa mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uwekezaji wa Umma na Fedha Maalum inayoongozwa na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, maafisa wa EACC walisema walipokea madai ya ukiukaji wa sheria za ununuzi na mgongano wa kimaslahi dhidi ya Bi Ngilu katika kuanzisha na kuendesha Kicotec.

Kiini cha shutuma hizo ni kuhusika kwa kampuni ya Trendy Links Limited, inayodaiwa kumilikiwa na mwana wa Bi Ngilu na kampuni hiyo.

Baada ya uchunguzi, EACC ilisema ilibainika kuwa Trendy Limited ilipewa kandarasi ya kuuzia kampuni hiyo, uagizaji na mafunzo ya ushonaji wa nguo.

Mkataba huo ulitiwa saini Mei 21, 2018 ukiwa kandarasi ya Sh66.4 milioni katika zabuni ya wazi iliyotangazwa Aprili 2018 huku Trendy ikiwa kampuni pekee iliyowasilisha zabuni.

Kulingana na EACC, uchunguzi ulionyesha zaidi kwamba Sh41.57 milioni zililipwa na serikali ya kaunti kwa Trendy Links kwa makundi kati ya Julai 2018 na Julai 2019.

“Tume ilikamilisha uchunguzi na kupeleka faili hiyo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma mnamo Julai 10, 2023 ikiwa na mapendekezo ya kuwafungulia mashtaka maafisa watano wa kaunti kwa makosa mbalimbali ya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi,” EACC ilisema.