Dereva wa teksi Victoria Mumbua alipigwa na kunyongwa hadi akafariki – Mtaalamu
DEREVA wa teksi aliyeuawa Victoria Mumbua Muloki ambaye mwili wake ulipatikana katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City katika kaunti ya Nairobi, alifariki baada ya kupigwa mara kwa mara kwa kifaa butu kabla ya kunyongwa hadi akafariki, uchunguzi wa maiti umefichua.
Uchunguzi huo ambao ulifanywa Jumatano na mtaalamu wa uchunguzi wa maiti wa serikali Dkt Johansen Oduor, pia ulifichua kuwa marehemu Mumbua alipambana na mshambuliaji wake ishara kwamba alijaribu kujilinda au kupigana.
Akizungumza kwa simu, Dkt Oduor alisema mama huyo wa watoto watatu pia alikuwa na majeraha mwilini.
“Kutokana na uchunguzi wangu, niligundua kwamba chanzo cha kifo cha Mumbua kilikuwa ni majeraha kadhaa, ambayo ni pamoja na jeraha kubwa la kichwa. Mshambuliaji alimpiga mara kadhaa kichwani. Zaidi ya hayo, mshambulizi baadaye alimnyonga hadi kufa. Pia kulikuwa na majeraha mikononi, kumaanisha kwamba alikuwa akijaribu kujilinda,” Dkt Oduor aliongeza.
Pia alisema alisema kuwa sampuli zilichukuliwa kwa uchunguzi zaidi kubaini iwapo alidhulumiwa kingono au kulishwa sumu.
“Familia ya marehemu inataka kujua ikiwa alilishwa sumu au alidhulumiwa kingono,” alisema.
Dereva huyo wa teksi mwenye umri wa miaka 35 kutoka kaunti ya Mombasa, alitoweka baada ya kumbeba mteja kutoka Mombasa hadi Samburu, Kaunti ya Kwale mnamo Septemba 27, na mwili wake kupatikana katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City, kaunti ya Nairobi.