Habari Mseto

Baba mng’ang’anizi alivyopoteza kesi ya nani wa kumzika mtoto aliyeuawa katika maandamano ya jenzii

Na GEORGE ODIWUOR October 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA ya Mbita imeamuru Kennedy Onyango, mvulana wa miaka 12 aliyeuawa Rongai kaunti ya Kajiado wakati wa maandamano ya kuipinga serikali mwezi Juni 2024 azikwe Rusinga.

Hii ni kinyume na matakwa ya babake marehemu Denish Okinyi ambaye alitaka mtoto huyo azikwe nyumbani kwake katika Kijiji cha Kisaku Suba, Kaunti ya Homa Bay.Katika uamuzi wake, Hakimu Mkuu wa Mbita, Martha Agutu aliagiza mwili wa marehemu upelekwe katika Kijiji cha Kamasengre, Rusinga.

Maagizo ya mahakama yalimaanisha kuwa marehemu atazikwa na mamake Jecinter Anyango.

Bw Okinyi na Bi Anyango walikuwa wanandoa lakini walitengana kwa sababu ya mizozo ya kifamilia kabla ya mwanamke huyo kuolewa na mwanamume mwingine Rusinga.

Baada ya kifo cha Onyango, wawili hao walianza kuzozania mwili wake.

Wote wawili walidai kuwa na haki ya kuuzika mwili huo.

Bi Anyango awali alifanya mipango ya mazishi na kuhamisha mwili hadi Homa Bay kutoka Nairobi, kwa nia ya kumzlka mwanawe.

Lakini mazishi hayo yalisitishwa na mahakama baada ya mwili huo kufika mjini Mbita.

Bw Okinyi alipata maagizo ya kusitisha mazishi hadi kesi hiyo iamuliwe.

Alitaka apewe mwili huo uzikwe nyumbani kwake.Awali, Hakimu aliwataka wahusika wawe na maelewano nje ya mahakama kukubaliana ni nani amzike mtoto huyo.

Lakini mchakato wa kusuluhisha suala hilo haukufaulu na ikabidi wawakilishe kesi hiyo tena mahakamani kusikilizwa.Mahakama ilibaini kuwa Bw Okinyi alikosa kutoa ushahidi kwamba alimuoa Bi Anyango.

Hapo awali, alikuwa ameambia mahakama kwamba alipeleka mahari kwa akina Anyango kwa kuzingatia mila za kitamaduni za Abasuba.Mahakama iliamua kwamba hakuna ushahidi wa kuonyesha alifanya hivyo.

Mahakama iliamua kuwa Bw Okinyi ndiye baba mzazi wa marehemu.Lakini Bi Agutu alisema hii haimpi haki ya moja kwa moja ya kuzika mwili hata kama sheria za kimila za Wajaluo zilisema hivyo.