Habari

Ruto anavyotekeleza ahadi ya kutuma polisi Haiti nchi zingine zikikosa kutekeleza ahadi zao

Na NYABOGA KIAGE October 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAAFISA 600 zaidi wa polisi, ambao wanaendelea na mafunzo, watatumwa Haiti kuanzia Novemba 2024 kama sehemu ya Kikosi cha Usalama cha Kimataifa (MSS).

Haya ni kwa mujibu wa tangazo ambalo lilitolewa na Rais William Ruto.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa wanahabari katika Ikulu ya Nairobi na Waziri Mkuu wa Haiti Garry Conille anayezuru Kenya, Rais Ruto alisisitiza kujitolea kwa Kenya kwa kikosi cha kimataifa kurejesha utulivu katika taifa hilo.

Dkt Conille alitua Kenya Alhamisi, Oktoba 10, 2024.

‘Jumla ya maafisa wa polisi 600 wa Kenya bado wanaendelea na mafunzo na watatumwa Haiti mwezi ujao,’ alisema Rais Ruto.

Kufikia sasa Kenya na Jamaica ndizo nchi ambazo zimetuma maafisa wao wa polisi nchini Haiti.

Nchi nyingine zilizoahidi kufanya hivyo na bado hazijatuma maafisa wao ni pamoja na; Bahamas, Antigua, Barbuda, Italia, Uhispania, Mongolia, Senegal, Belize, Suriname, Guatemala na Peru.

Ziara ya Waziri Mkuu wa Haiti inajiri wiki tatu tu baada ya Rais William Ruto kuzuru taifa hilo.

Wakati wa ziara ya hivi majuzi nchini Haiti, Rais Ruto alisema kwamba anaunga mkono kugeuzwa kwa kikosi hicho kuwa cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa (UN).

Maafisa hao pia walielezea changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo wakiwa Haiti huku wakisema hasa wanahitaji rasilimali zaidi ambazo zitawasaidia kurejesha amani huko.