• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 4:48 PM
Magaidi hawana dini wala kabila – SUPKEM

Magaidi hawana dini wala kabila – SUPKEM

CECIL ODONGO na MOHAMED AHMED

VIONGOZI wa Baraza kuu la Kiislamu nchini (SUPKEM) Jumatano walikemea wanaohusisha magaidi waliotekeleza shambulizi katika hoteli ya Dusit D2 mtaani Riverside na dini ya Kiislamu, wakisema magaidi hawana dini au kabila.

Wakizungumza kwenye kikao na wanahabari katika Msikiti wa Jamia jijini Nairobi, viongozi hao walisema msingi wa dini ya Kiislamu ni amani na mafundisho ya kitabu kitakatifu cha Koran yanakemea sana mauaji au umwagikaji wa damu.

“Tunakemea kwa kinywa kipana shambulizi la Riverside ila haifai kwa baadhi ya Wakenya kuzamia mitandao ya kijamii na kudai kwamba Waislamu ndio walihusika. Sisi tunahubiri amani na dini yetu inakataa mauaji,” akasema Naibu Mwenyekiti wa SUPKEM, Al-Haji Hassan Ole Nado.

Kauli yake iliungwa mkono na Imam wa Msikiti wa Jamia Sheikh Mohamed Swalhu ambaye alizipa faraja familia zilizoathirika na kusema kwamba wamefungua kituo kikuu cha kutoa damu katika hospitali ya Chiromo ili kuwasaidia waathiriwa.

“Tunawapa faraja na kuwaombea wote walioathirika ila sisi ni wenye amani na wanaohusisha dini yetu na ugaidi wanakosea sana. Tumefungua kituo cha kutoa damu na tunawaomba waomba Waislamu na Wakenya wengine wafike huko ili kutoa damu.

Mjini Mombasa, mwasisi wa Umoja wa Wasomi wa Afrika, Sheikh Abu Hamza alikariri wito wa wenzake kwa kusema matukio ya kigaidi hayalingani na mafunzo ya dini ya Kiislamu.

Alisema wanaalani kitendo hicho.

“Kisa hiki kimesababisha maafa kwa watu wengi. Hakuna katika vitabu vyetu vitukufu maelezo yoyote yanayoruhusu majambazi hawa,” akasema Sheik Hamza.

Msomi huyo pia aliwapongeza maafisa wa usalama kwa kutekeleza kazi nzuri ya kupambana na magaidi hao aliowataja kuwa ‘maadui’ wa nchi.

“Tumeona kuwa vyombo vyetu vya usalama vimetekeleza kazi nzuri na ni muhimu kwetu sisi kuwapa kongole kwa kazi hiyo. Hii yote ni juhudi bora ya serikali kupambana na uhalifu,” akaongeza.

You can share this post!

Wakulima watapeliwa mamilioni na watu waliojifanya kutoka UN

TAHARIRI: Waliokabili magaidi fahari kwa Kenya

adminleo