Habari za Kitaifa

Jinsi masanduku 12 ya ushahidi wa Gachagua yalivyoibua kumbukumbu ya kesi za Azimio

Na MARY WANGARI October 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais, Rigathi Gachagua, Jumatatu aliwasilisha ushahidi wake kwa Seneti kabla ya vikao vya kusikiza mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yake vilivyopangiwa kufanyika Jumatano na Alhamisi.

Bw Gachagua aliwasilisha masanduku 12 ya ushahidi kupitia mawakili George Sakimpa na Eric Naibei, ambao ni miongoni mwa timu ya mawakili 14 wanaomwakilisha Naibu Rais.

Karani wa Bunge la Seneti Jeremiah Nyengenye alikabidhiwa ushahidi huo uliosafirishwa kwa gari aina ya pickup kutoka Bungeni, na mwenzake wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge.

Wahudumu wa bunge kisha walikagua ushahidi huo kuhakikisha kila kitu kiko shwari kabla ya maseneta kuanza kusikiza madai yaliyowasilishwa dhidi ya Naibu Rais kupitia hoja ya kumng’oa mamlakani.

Haya yalijiri huku Mahakama Kuu ikitazamiwa kutoa uamuzi hii leo (Jumanne) kuhusu kesi iliyowasilishwa na Bw Gachagua akitaka kusimamisha mchakato wa Seneti.

Jana, Jaji Mkuu Martha Koome aliteua jopokazi la majaji watatu kusikiza kesi sita zinazopinga hoja ya kumfurusha Naibu Rais.

Majaji Eric Ogolla, Antony Mrima na Frida Mugambi wanatazamiwa kushughulikia suala hilo.

Mchakato wa kumtimua Bw Rigathi ambao umeonekana kuendeshwa kwa kasi ya ajabu ulifika Seneti Alhamisi siku moja baada ya wabunge 282 kupiga kura kuunga mkono hoja ya kumfurusha ikilinganishwa na 44 waliopinga.

Spika wa Seneti Amason Kingi aliagiza mashtaka dhidi ya Bw Gachagua yasikizwe katika kikao cha maseneta wote baada ya pendekezo la kuunda kamati maalum ya maseneta 11 kushughulikia suala hilo, kukosa kungwa mkono inavyohitajika na kanuni za Seneti.

Katika kikao cha Seneti Jumatano, Naibu Kiranja wa Wachache, Edwin Sifuna alipinga pendekezo hilo lililowasilishwa na Kiongozi wa Wengi, Aaron Cheruiyot, akisema, “Hili ni suala la kipekee ambalo limevutia umma pakubwa.”

“Kwa mara ya kwanza Seneti imealikwa kuendesha vikao vya kusikiza hoja ya kumfurusha Naibu Rais. Japo ni mchakato wa kikatiba, ni mara ya kwanza haya yanatendeka. Tuna njia mbili kulingana na kanuni za seneti. Ama kuchagua maseneta 11 kusikiza hoja hii na kutushauri kupitia kamati maalum au kusikiza katika kikao kinachojumuisha maseneta wote,” alieleza Seneta Cheruiyot.

Ikiwa korti itaruhusu mchakato wa Seneti kuendelea, Naibu Rais atatimuliwa ikiwa thuluthi mbili ya maseneta wote 67 sawa na maseneta 44, watapiga kura kuunga hoja ya kumfurusha.

Katika kikao Jumanne, Spika Kingi aliwahakikishia kuwa Seneti imejitolea kutekeleza haki huku akiwaonya maseneta dhidi ya kujadili lolote kuhusu mchakato huo.

Aidha, Spika alisimamisha safari zote za maseneti nje ya nchi hadi hoja hiyo isikizwe na kuamuliwa.

“Mchakato tunaoelekea kuanza si rahisi. Taifa na ulimwengu unatazama. Nidhamu ni muhimu sana baina ya maseneta,” alisema Spika Kingi.

“Baada ya kusoma mashtaka tuna siku 10. Nimeagiza suala hili lisikizwe katika muda wa siku mbili. Tutakapoona orodha ya mashahidi na kubaini hatuwezi kumaliza suala hili kwa siku mbili, tuna Ijumaa.”