Ni ‘luwere’ Harambee Stars ama bado? Wameng’atwa tena na Cameroon
HARAMBEE Stars imepoteza alama zote tena dhidi ya Cameroon katika mechi ya mkondo wa pili ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2025 baada ya kuchapwa 1-0 ugani Nelson Mandela nchini Uganda, Jumatatu, Oktoba 14, 2024.
Vijana wa kocha Engin Firat waliokubali kipigo cha mabao 4-1 katika mkondo wa kwanza mjini Yaounde mnamo Oktoba 11, wamezamishwa na bao la Boris Enow. Enow alipachika kutokna na frikiki dakika ya 63.
Firat alitumia mfumo wa 4-3-3 aliwaanzisha Bryne Omondi (kipa), Daniel Anyembe, Joseph Okumu, Johnstone Omurwa na Eric Ouma katika safu ya ulinzi, Duke Abuya, Anthony Akumu na Richard Odada katika safu ya katikati nao Ronney Onyango, nahodha Michael Olunga na John Avire wakatwikwa majukumu ya kufanya mashambulizi.
Marc Brys wa Cameroon alitumia mfumo wa 4-1-4-1, huku Andre Onana akilinda lango naye nahodha Vincent Aboubakar akiongoza mashambulizi.
Kenya, ambayo itashirikiana na Tanzania na Uganda kuandaa AFCON mwaka 2027, inasalia katika nafasi ya tatu kwenye Kundi J kwa alama nne baada ya kujibwaga uwanjani mara nne.
Indomitable Lions ya Cameroon inaongoza kundi kwa alama 10 ikifuatiwa na Zimbabwe itakayoalika Namibia baadaye Oktoba 14 katika mechi yao ya nne. Zimbabwe ina alama tano. Namibia inavuta mkia bila alama.
Kenya sasa itamenyana na Zimbabwe (Novemba 11 ugenini) na Namibia (Novemba 19 nyumbani) katika mechi zake mbili za mwisho. Kuna makundi 12 ambapo washindi na nambari mbili kutoka kila kundi watajikatia tiketi kushiriki AFCON2025 nchini Morocco.
Morocco wamefuzu moja kwa moja nao Burkina Faso na Cameroon wamefuzu kwa kujihakikishia watamaliza makundi yao katika nafasi ya pili bila ya kujali matokeo ya mechi mbili za mwisho.
Mara ya mwisho Kenya ilishiriki AFCON ni mwaka 2019 nchini Misri. Harambee Stars itafanikiwa tu kuingia AFCON 2025 ikiwa Zimbabwe itapoteza mechi zake tatu ilizo nazo.