Meya wa Tanzania: Vijana wa Kenya mkifanya vurugu za maandamano zinatuathiri hadi Tanga
MEYA kutoka Tanzania amewataka vijana nchini Kenya kujiepusha na shughuli zinazoweza kuliweka taifa katika hali mbaya.
Meya huyo wa jiji la Tanga Abdurahman Shiloow aliwaomba vijana kumakinika na kuepuka kutumika vibaya na watu fulani waliokuwa na nia mbaya kwa nchi.
Kulingana na Bw Shiloow, nafasi ya kimkakati inayomilikiwa na Kenya katika ukanda wa Afrika Mashariki, inafanya taifa jirani kuathirika, endapo kuna lolote baya linalotokea.
Matamshi yake yalionekana kuzungumzia maandamano ya vijana wa Gen Z yaliyofanyika miezi ya Juni na Julai na kulazimisha Mswada wa Fedha 2024 uliokuwa unapingwa kwa kusheheni ushuru mpya kufutwa na Rais William Ruto.
“Mimi ni mwanasiasa, na kama jirani zenu, naweza kuwaambia kuwa endapo lolote litakwenda mrama hapa nchini, hata sisi tutahisi tukiwa Tanga. Mambo yakiwa mazuri, tunahisi pia,” akasema Bw Shiloow.
Meya huyo alikuwa akizungumza katika siku ya pili ya awamu ya tano ya wiki ya Uvumbuzi Mombasa.
“Chochote tunachofanya tufanye kwa amani na tuepuke mgawanyiko. Nyinyi vijana, ndio nguvu na raslimali ya kaunti ya Mombasa na Kenya, ila mnapaswa kutumika kwa njia sawa. Msikubali kutumika vibaya kwa madhumuni mabaya.”
“Hakuna nchi nyinginme wala kaunti nyingine, kwa hivyo fikirieni kufaulu kwenu na fanyeni kazi kuhakikisha kuwa Mombasa na Kenya zinang’aa kwa sababu ya juhudi zenyu. Nimeongea lugha ya watu werevu ila huko kwetu unapozungumza mambo yanayowahusu watu wengi tunazungumza Kiswahili. Tukiwakaribisha kule kwetu pia sisi tutawasilisha kila kitu kwa Kiswahili,” akaongeza.
Wazungumzaji katika hafla hiyo walitoa wito kwa vijana kutoka Pwani kukumbatia uvumbuzi kama njia ya kukabiliana na suala la ukosefu wa ajira na kutafuta suluhu kwa mambo muhimu yanayokumba jamii.
Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana kutumia talanta na ubunifu wao kujisakia tonge.
“Naelewa umuhimu wa hafla kama hizo. Kukiwa na hitaji la kitu, watu hutafutwa kulishughulikia. Kwa hivyo, iwapo vijana watatumia uvumbuzi na ubunifu, kazi zinazohitaji ujuzi huo zitapatikana. Tayari tumefanya kazi na vijana kuhamihsia huduma zetu Mtandaoni,” akasema Bw Nassir.