HIVI PUNDE: Teke la mwisho: Maseneta wapiga kura kumfuta kazi Naibu Rais Rigathi Gachagua
MASENETA wamepiga kura ya kumtimua mamlakani Naibu Rais Rigathi Gachagua, miaka miwili pekee tangu kusaidia kuunga serikali ya Kenya Kwanza.
Katika kura kuhusu mashtaka 11 ambayo alishtakiwa nayo, zaidi ya nusu yalipata ‘NDIO’ huku upigaji kura ukiendelea kufikia wakati wa kuandika taarifa hii.
Kisheria, kiongozi anahitajika tu kupatikana na hatia ya kosa moja kwake yeye kutangazwa kwamba ameng’atuliwa uongozini.
Awali, mawakili wake, wakiongozwa na Wakili Mkuu Paul Muite, Alhamisi alasiri waliarifu Seneti kwamba Bw Gachagua, ambaye alihudhuria vikao vya Jumatano na Alhamisi asubuhi, amelazwa katika hospitali ya Nairobi, na hakuweza kupatikana ili kuhojiwa.
Alikuwa amejiorodhesha kama shahidi pekee kwenye kesi hiyo baada ya kuamua kutojumuisha mashahidi wengine kumtetea.
“Ilivyo ni kwamba nilipojaribu kumtafuta, ukweli wa kusikitisha ni kwamba Naibu Rais amekuwa mgonjwa na ninavyozungumza sasa, yuko hospitalini,” Bw Muite aliambia Seneti.
“Nipe muda uliobakia wa siku niangalie hali yake na nirudi hapa saa kumi na moja jioni.”
Baada ya mapumziko ya chakula cha mchana, Naibu Rais alitakiwa kuingia kizimbani kuhojiwa na mawakili wa Bunge.
Mawakili wa Bunge la Kitaifa walimuomba Spika Amason Kingi atoe uamuzi kuhusu suala hilo, wakisema kesi ya kumuondoa mamlakani imewekewa wakati wa kuikamilisha.
“Haya mashauri yamepitwa na wakati. Sio kuhusu hali ambayo Naibu Rais amejipata lakini ni kuhusu Seneti kutii masharti ya Katiba ambayo lazima ifanye uamuzi ndani ya muda fulani,” Wakili Mkuu James Orengo alisema.
Bw Kingi alisimamisha shughuli za Seneti kwa saa moja na akaagiza Bunge hilo likutane tena kuanzia saa kumi na moja jioni.
“Kikao hiki kimeahirishwa hadi saa kumi na moja jioni wakati Naibu Rais atakapotarajiwa kufika kizimbani. Huu ni mchakato wa muda. Nimeamua hivyo,” alisema.