Wasifu wa Naibu Rais Mteule Kithure Kindiki
KABLA ya kuteuliwa Waziri na Naibu Rais, Profesa Kithure Kindiki alihudumu kama Seneta wa Kaunti ya Tharaka Nithi, kuanzia 2013, ambapo pia alihudumu kama Naibu Spika wa Seneti; pamoja na Kiongozi wa Wengi katika Seneti.
Akiwa Kiongozi wa Wengi katika Seneti, aliongoza ajenda ya kutunga sheria ya chama cha wengi katika Seneti.
Kindiki pia amefundisha sheria na kushikilia nyadhifa mbalimbali za utawala katika kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Moi na kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Nairobi.
Alianza taaluma yake kama Mhadhiri Msaidizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Moi punde tu baada ya kuhitimu na shahada ya kwanza ya sheria.
Kisha alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kama Mhadhiri baada ya kuhitimu Shahada ya Uzamifu katika Sheria ya Kimataifa ambapo alipandishwa cheo haraka hadi Mkuu wa Idara ya Sheria ya Umma akiwa na umri wa miaka 33 na kisha kuwa Msimamizi Msaidizi akiwa na umri wa miaka 35.
Baadaye Kindiki alipandishwa cheo kuwa Profesa Mwandamizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Ameandika machapisho thelathini na matano yakiwemo vitabu, sura za vitabu na makala katika majarida nchini na kimataifa.
Profesa Kindiki ana Shahada ya Kwanza ya Sheria (LL.B) kutoka Chuo Kikuu cha Moi, Diploma ya Uzamili ya Sheria kutoka Shule ya Sheria ya Kenya, Shahada ya Uzamili ya Sheria (LL.M), na Shahada ya Uzamifu (Ph.D.) katika sheria ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini.
Aliwakilisha Rais Ruto katika kesi iliyomkabili katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008.