Habari Mseto

KEPSA yakemea vikali mauaji ya 14 Riverside

January 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Chama cha wamiliki biashara wa kibinafsi kimekemea vikali shambulizi la kigaidi 14 Riverside, Nairobi.

Shambulizi hilo la Jumanne lilipelekea vifo vya watu kufikia 15 na kusababisha majeruhi wengi.

Katika taarifa, chama hicho kilisema kuwa wananchi wa Kenya hawatahofishwa na hatua za kigaidi kama hiyo iliyolenga kutatiza sekta ya kibinafsi.

Jumba la Dusit 2, lililoshambuliwa na magaidi hayo limehifadhi afisi nyingi za kitaifa, kimataifa na kibinafsi, baadhi yake wanachama wa KEPSA.

“Biashara na mashirika hayo yameajiri wananchi wengi na shambulizi hilo lilisababisha hofu isiyo muhimu. Sekta ya kibinafsi ndio injini ya uchumi wa Kenya kwani inabuni nafasi za kazi na kutoa ushuru wa kujitegemea na kushambulia sekta hii ni kuua matumaini ya kesho,” ilisema KEPSA.

Sekta hiyo ilipongeza vikosi vya usalama vilivyofika eneo hilo na kudhibiti hali pamoja na kuwaokoa wote waliofumaniwa humo.

“Tunapongeza maafisa wengine wa usalama waliohakikisha kuwa biashara imeendelea kwingineko na kuwahakikishia wananchi kuwa hali ilikuwa imedhibitiwa,” chama hicho kilisema.