Makala

Dalili za wazi, hatari alizozipuuza Gachagua

Na BENSON MATHEKA October 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua alipuuza dalili za wazi kwamba angeondolewa ofisini, tayari alionyeshwa ishara na mkubwa wake Rais William Ruto na wabunge hasa wa kutoka ngome yake ya Mlima Kenya.

Akiwa na azma ya kuwa msemaji wa Mlima Kenya, Bw Gachagua huenda alipofushwa na mamlaka akakosa kuona pia mitego aliyowekewa na ambayo iliunda sehemu ya mashtaka ya kumwondoa mamlakani.

Wadadisi wa siasa wanasema mikakati ya kumtimua Bw Gachagua ilisukwa kwa siri kubwa huku baadhi ya wabunge wakitumiwa kutoa ishara mara kwa mara ambazo kwa kulewa na mamlaka hasa kwa kuwa ngome yake ya Mlima Kenya ilimpa Rais Ruto kura nyingi, Bw Gachagua alipuuza.

Miongoni mwa dalili hizo ni wabunge wa Kenya Kwanza kumkosoa hadharani licha ya kuwa walipaswa kumheshimu akiwa naibu kiongozi wa chama na kusitishwa kwa uchaguzi wa chama cha UDA ambao aliingilia kati katika juhudi za kutaka kupanda vibaraka wake katika nafasi muhimu na kutofahamishwa hafla na shughuli za rais licha ya kuwa msaidizi wake mkuu.

Bw Gachagua, katika mojawapo ya mikutano na wanahabari baada ya kubaini chuma chake kilikuwa  motoni, alifichua kuwa alikuwa ameondolewa katika kundi la WhatsApp la maafisa wakuu wa Ikulu na hakuweza kujipanga kuhudhuria hafla rasmi za kiongozi wa nchi.

“Dalili za wazi ambazo alipuuza na ambazo zilitolewa baada ya mikakati ya kumtimua kuiva kiasi kwamba hakukuwa na kurudi nyuma zilikuwa kutengwa kwake na wabunge wa Mlima Kenya waliomwidhinisha Waziri Kithure Kindiki kuwa msemaji wao.

Kwa hakika, walitumia neno kuwa Kindiki angekuwa “kiunganishi chao na serikali,” akasema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Wabunge kutoka kaunti za Tharaka Nithi, Embu na Meru, zilizoko eneo la Mlima Kenya Mashariki walikuwa wa kwanza kumtema Bw Gachagua na kuegemea Profesa Kindiki, hatua ambayo mbunge huyo wa zamani wa Mathira alipuuza bila kujua ilikuwa sehemu ya mikakati mipana ya kummaliza kisiasa huku akisisitiza kuwa angetishika.

Siku chache baadaye dalili kwamba angebanduliwa mamlakani zilijitokeza tena wabunge 48 kutoka kaunti za Mlima Kenya Mashariki walipokutana katika hoteli moja Nyandarua na kuunga hatua ya wenzao wa Mlima Kenya Magharibi kuegemea Profesa Kindiki kama msemaji wa eneo lao.

“Kufikia wakati huu ilimbainikia Bw Gachagua kuwa mambo hayakuwa sawa kwa kuwa wabunge washirika wake walikuwa wakiandamwa na idara za upelelezi kwa madai ya kufadhili maandamano ya vijana yaliyotikisa nchi. Bw Gachagua alilalamika vikali akidai lengo lilikuwa ni kumhusisha yeye na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na maandamano hayo.

“Kufikia wakati huu, mikakati ya kumbandua mamlakani ilikuwa imeiva na lilikuwa suala la ni lini hoja ingewasilishwa bungeni,” akasema Dkt Gichuki.

Kulingana na mchambuzi wa siasa Dkt Irene Kariuki, dalili kuu kabisa ambayo Bw Gachagua alipuuza ni ukuruba wa kisiasa kati ya Rais Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga ambao, kulingana na alivyoaminishwa, ulinuiwa kuunganisha nchi.

Dkt Kariuki anasema ushirika wa Rais Ruto na mpinzani wake mkuu katika uchaguzi mkuu wa 2022 uliobatizwa Serikali Jumuishi ulinuiwa kupata idadi ya kutosha ya wabunge kuunga hoja ya kumtimua mamlakani Bw Gachagua.

Ni baada ya mikakati kuiva ambapo Rais Ruto anasemekana alianza kumkemea Bw Gachagua akimlaumu kwa kwenda kinyume cha makubaliano ya pamoja ya serikali na kuhujumu serikali kwa kupanga uchaguzi mkuu wa 2027.

Inasemekana kabla ya ziara yake ya kuelekea China mnamo Septemba 2024, Rais Ruto alimkemea vikali Bw Gachagua mbele ya maafisa wa ngazi za chini wakiwa katika uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta.

Japo katika vikao vyake na wanahabari kabla ya hoja ya kumwondoa mamlakani hakukiri kisa hicho, Bw Gachagua alisema afisa mmoja mkuu serikalini alimwita mjinga.

Dkt Kariuki anasema kuwa hizi ni baadhi ya dalili ambazo Bw Gachagua alipuuza.

“Zilikuwa wazi. Hata rais alisema akiwa Nyeri kwamba watu wakome kuendeleza siasa za 2027 kwa kuwa Mungu anaweza kupanga vingine. Sasa, baada ya Gachagua kuondolewa mamlakani, hataweza kugombea kiti chochote katika uchaguzi huo,” akasema Kariuki.