Makala

Gachagua aanza kuhisi baridi

Na CHARLES WASONGA October 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais aliyetimuliwa afisini Rigathi Gachagua, ameanza kuhisi baridi baada ya serikali kumpokonya baadhi ya walinzi, wafanyakazi wake kupewa likizo ya lazima huku picha na taarifa zake zikiondolewa katika tovuti ya Afisi ya Rais na Ikulu.

Mnamo Jumamosi, jumla ya wafanyakazi 108 walioajiriwa mahsusi kumhudumia waliagizwa kuondoka kufikia adhuhuri, kutokana kile kinachodaiwa kuwa “mchakato wa kikatiba unaoathiri naibu rais.”

Aidha, duru zilisema kuwa wafanyakazi wote wa serikali waliokuwa wakihudumu katika boma la Bw Gachagua, lililoko kijiji cha Wamunyoro, eneo bunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri, waliagizwa waondoke Ijumaa asubuhi.

Hatua hiyo ilijiri saa chache baada ya Seneti kuidhinisha hatua ya Bunge la Kitaifa ya kumwondoa afisini, Alhamisi usiku.

Wafanyakazi walioondolewa ni pamoja na wapishi na maafisa wa usalama waliokuwa wakilinda boma hilo.

Waliagizwa kuondoka mnamo Ijumaa saa kumi na mbili alfajiri.

Magari rasmi ya Bw Gachagua pia yalitwaliwa.

Isitoshe, Taifa Jumapili ilibaini kuwa picha na taarifa zote kuhusu Bw Gachagua ziliondolewa kutoka tovuti ya Afisi ya Rais na Ikulu; sawa na katika majukwaa ya mitandao ya kijamii ya asasi hizo.

Maelezo hayo yalikuwepo kwenye majukwaa hayo kabla ya Seneti kuidhinisha kutimuliwa afisini Alhamisi usiku.

Hatua hizo ilichukuliwa hata kabla ya kuanza kwa mchakato wa kusikizwa kwa kesi kadha zilizowasilishwa katika Mahakama Kuu kusimamisha, kwa muda, kujazwa kwa nafasi ya Bw Gachagua na Kithure Kindiki.

Profesa Kindiki, ambaye ni Waziri wa Usalama wa Ndani, alipendekezwa na Rais William Ruto na kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa katika kikao cha Ijumaa.

Kisha Spika Moses Wetang’ula akamtangaza Naibu Rais Mteule kupitia chapisho kwenye toleo maalum la gazeti rasmi la serikali.

Lakini katika agizo lake siku hiyo hiyo, Jaji Chacha Mwita aliagiza kuwa shughuli ya kujazwa kwa nafasi ya Bw Gachagua, isitishwe hadi Oktoba 24, kesi yake itakaposikizwa na jopo la majaji watakaoteuliwa na Jaji Mkuu Martha Koome.

Agizo sawa na hilo lilitolewa na Jaji Richard Mwongo wa Mahakama Kuu ya Kerugoya.

Maagizo hayo ndiyo yalichangia kuahirishwa kwa sherehe ya kumwapishwa Profesa Kindiki iliyopangwa kufanyika Ijumaa katika uwanja wa Jamhuri Park na kuongozwa na Bi Koome, kulingana na kipengele cha 148 cha Katiba.

Mnamo Jumamosi, Mbunge Mwakilishi wa Kirinyaga Janes Njeri Maina alikosoa hatua ya serikali kuwaondoa walinzi wa Bw Gachagua na kuwatuma likizoni wafanyakazi wake.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Gachagua aliitaka serikali kuwaruhusu wafanyakazi hao kuendelea na kazi hadi kesi zilizowasilishwa kortini zitakaposikizwa na kuamuliwa.

“Kile serikali imefanya ni kinyume cha sheria, wafanyakazi hao wanapaswa kusalia kazini hadi kesi zilizoko mahakamani zitakaposikizwa na uamuzi kutolewa,” Bi Maina akasema, akiisuta serikali kwa kuendelea kumtesa Bw Gachagua hata wakati huu ambapo amelazwa hospitalini.

Kwa upande wake, Mbunge wa zamani wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu akisema hivi: “Ukweli ni kwamba Wakenya wote wanafahamu kwamba kile ambacho serikali inamfanyia Rigathi Gachagua sio sawa na ni hatari sio tu kwake bali kwetu sote.”

Bw Ngunjiri, ambaye amekuwa akihudumu kama mshauri wa kisiasa katika afisini ya Naibu Rais ni miongoni mwa wafanyakazi 108 waliondolewa.

Wengine ni Mbunge wa zamani wa Embakasi Magharibi George Theuri aliyekuwa akihudumu kama mshauri wa kuhusu masuala ya vijana.

Bi Elizabeth Wanjiku, ambaye amekuwa akihudumu Mkuu wa Wafanyakazi katika Afisi ya Naibu Rais pia ni mwathiriwa.