Makala

Kivuli cha Raila katika utimuaji wa Gachagua

Na BENSON MATHEKA October 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga, anaonekana kupiga jeki kuondolewa kwa Bw Rigathi Gachagua kama naibu rais wa Kenya nyuma ya pazia licha ya kutangaza kuwa asingehusika na siasa za nchini akiendeleza kampeni yake ya uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

Mbali na wabunge na maseneta wengi wa chama chake kuunga hoja hiyo, baadhi yao ambao ni mawakili wa hadhi ya juu waliwakilisha Bunge kumshtaki Bw Gachagua katika seneti na hawakuficha msimamo wao katika mchakato huo wakiutaja kama wa kisiasa.

Kuungana kwa wabunge wa ODM na wale wa muungano wa Kenya Kwanza walio waaminifu kwa Rais Ruto pia kulichangia pakubwa kuondolewa mamlakani kwa Bw Gachagua huku wadadisi wa siasa wakisisitiza kuwa bila ukuruba wa kisiasa wa Bw Odinga na kiongozi wa nchi, ingekuwa vigumu kupata idadi ya kutosha kuunga hoja hiyo.

Wabunge 282 waliunga hoja ya kumtimua Bw Gachagua mamlakani na 236 wakaidhinisha uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki kujaza nafasi iliyoachwa wazi.

Wabunge wa muungano wa Kenya Kwanza hawazidi 165. ODM ina wabunge 82.Maseneta wa ODM, pia waliungana na wale wa Kenya Kwanza kumpata Bw Gachagua na hatia ya mashtaka matano kati ya 11 yaliyokuwa katika hoja iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.

“Ulikuwa mchakato wa kisiasa na kwa wabunge wa ODM kuhusika kikamilifu lazima walikuwa na baraka za kiongozi wa chama chao. Kujitokeza kwa viongozi wa ODM ambao ni mawakili wakiwemo gavana wa Siaya Bw James Orengo, wabunge Otiende Amollo na Zamzam Mohamed kuwakilisha bunge ni ishara za wazi ya mkono wa Raila katika hoja ya kumtimua Bw Gachagua,” alisema mchambuzi wa siasa Joseph Kisilu.

Wakichangia katika mjadala wa hoja ya kumwondoa Bw Gachagua mamlakani, wabunge walitaja mchakato huo kuwa wa kisiasa huku Bw Mutuse akisema hata hakuhitajika kuthibitisha madai kikamilifu.

‘Wazo la kuondolewa mamlakani ni la kisheria lakini la kisiasa katika maudhui na ufaafu. Maadamu michakato ya kisheria ya kusikilizwa inazingatiwa, hakuna anayefaa kukosoa uhalali wa maamuzi ya Bunge au Seneti hii,” alisema Bw Amollo.

Wadadisi wanasema japo ni mchakato wa kisiasa unaoendesha katika bunge, unaongozwa na wanasiasa wakuu ambao sio wabunge.“Raila alihusika katika masaibu ya Gachagua kwa kuwa wabunge wa chama chake walionekana kufuata maagizo ya kuungana na wale wa Kenya Kwanza.

Haikuwa hivyo kwa wabunge wa vyama vingine vya upinzani na hii inaashiria mipango ya kuendelea kwa ushirika wake na Rais Ruto hadi uchaguzi mkuu wa 2027 na baadaye,” akasema Bw Kisilu.

Mnamo Ijumaa, kaimu kiongozi wa ODM, Profesa Anyang Nyong’o alisema chama hicho kinaweka mikakati ya kuunda miungano mipya itakayohakikisha kitakuwa katika serikali ijayo.Alisema chama hicho kinaangazia kwa dhati kufufua mikakati yake ya mashinani na kitaifa huku kikijijenga upya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.

‘Mkakati huu unaweza kutusaidia kupata tena uungwaji mkono na nguvu katika uchaguzi ujao. Kwa kushughulikia masuala ya ndani na kuimarisha mawasiliano yetu, ODM inatumai kuimarisha jukumu lake katika kuunda mustakabali wa kisiasa wa Kenya,” akasema.

Wadadisi wanasema kwamba hatua ya Bw Odinga kuunga mikataba tata ya kampuni ya Adani ambao Bw Gachagua anapinga inaonyesha kuhusika kwake katika mchakato huo.