SHAMBULIO: Serikali itagharamia matibabu ya waathiriwa wote – Ruto

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto ametangaza kuwa hospitali ambako waathiriwa wa shambulio katika eneo la 14 Riverside zimekubali serikali kugharamia matibabu ya waathiriwa wa shambulio hilo la kigaidi.

Akiongea Alhamisi jioni baada ya kuwatembelea waathiriwa waliolazwa katika hospitali mbalimbali jijini Nairobi wakipokea matibabu, Ruto alipongeza hospitali hizo kwa kujitolea kubeba mzigo wa gharama ya matibabu ya wahasiriwa wasio na bima ya matibabu.

“Ni furaha yangu kutangaza kwamba hospitali husika zimekubali kulipa gharama ya matibabu ya wahanga ambao hawana bima ya afya,” akasema alipoongea na wanahabari Jumatano katika hospitali ya Avenue.

Dkt Ruto kwa mara nyingine alitumia fursa hiyo ku tuma risala za rambi rambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao katika shambulio hilo. Aliwatakia afueni ya haraka.

“Natuma rambirambi zangu kwa familia na marafiki waliopoteza wapendwa wao katika shambulio hilo la woga katika majengo ya 14 Riverside. Nawatakia waliojeruhiwa uponyaji wa haraka. Ningependa kuwahakikishia kwamba serikali italipa bili za hospitali za waathiriwa wote,” naibu rais akasema katika ujumbe kupitia mtandao wa Twitter.

Mnamo Jumatano jioni serikali kupitia Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet alitangaza kuwa idadi ya waliofariki katika shambulio hilo imapanda hadi kufikia watu 21.

Bw Boinnet alisema miili sita ilipatikana katika eneo la mkasa.

“Mmoja wao wa waliofariki ni afisa wa polisi ambaye alifariki kutokana na majeraha aliyopata,” akasema Boinnet kwenye kikao na wanahabari Jumatano jioni.

Waliofariki ni; Wakenya 16, Mwingereza mmoja, Mwamerika mmoja na watu wengine watatu wa asili ya Afrika ambao bado hawajatambuliwa.

Habari zinazohusiana na hii