Bomoa bomoa yafikia familia 200 za kijiji cha Kirogo, Kirinyaga
SERIKALI imewatimua zaidi ya familia 200 kutoka kwa ekari 200 za ardhi ambazo zinamilikiwa na Shirika la Utafiti kuhusu Kilimo na Ufugaji (KALRO) kwenye kijiji cha Kirogo, Kaunti ya Kirinyaga.
Ubomozi huo ulifanyika mnamo Jumamosi asubuhi huku nyumba za wakazi kadhaa ikiharibiwa baada ya kuangushwa na trekta. Mimea ya familia kadhaa pia iliharibiwa wakati wa shughuli hiyo ambayo iliendelezwa na polisi waliokuwa wamejihami vikali.
Familia hizo zilisema zimeishi kwenye ardhi tangu miaka ya 90 na wakashutumu serikali kwa kuwaondoa kwa njia haramu.
“Tulinunua ardhi hii na kuishi ndani. Tuna vyeti vya umiliki ardhi na inasikitisha kuwa maafisa wa serikali walikuja na kuanza kuangusha nyumba zetu kisha kuharibu mimea,” akasema Bi Wanjiru Mwangi.
Familia kadhaa zililalamika kuwa zilipata hasara kubwa na zikaahidi kuwa zitashtaki serikali ilizilipwe fidia.
“Tumekuwa tukiishi kwenye ardhi hii kwa miaka mingi na hatuna kwingine pa kuita nyumbani. Hata tumewazika jamaa zetu hapa na makaburi yao yameharibiwa. Inashangaza kuwa serikali sasa inawashughulikia kwa njia hii,” akasema mkazi mwengine Bedan Murigu.
Irene Wawira naye alisimulia jinsi alivyofika katika shamba lake na kupata mpunga na maharagwe yakiwa yamengólewa.
Afisa mmoja wa KALRO ambaye hakutaka jina lake linukuliwe kwa kuwa haruhusiwi kuongea na wanahabari alisema familia hizo zilitupwa nje kutokana na amri ya mahakama.
“Tuna amri ya korti na familia hizo lazima zingeenda,” akasema.
Aliongeza kuwa familia hizo zilipewa notisi ya kuondoka kwenye ardhi hiyo lakini zikapuuza. Alisema ardhi hiyo ilikuwa ya kufanya utafiti wa kilimo lakini ikanyakuliwa mnamo 1995 kisha ikapewa familia hizo kwa njia haramu.
“Familia hizo zilikalia ardhi hiyo zikifahamu kuwa ni ya KALRO na sasa lazima wakome kulalamika,” akasema afisa huyo.
Kulikuwa na taharuki kwenye ardhi hiyo wakati ambapo maafisa wa usalama walipiga doria wakiwa tayari kukabiliana na fujo zozote ambazo zingezuka.