Habari za Kitaifa

Wakenya wanaoishi ng’ambo waelezea kutofurahia mienendo ya kisiasa humu nchini

Na MARY WANGARI October 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wanaoishi ughaibuni wametishia kushirikisha washirika wa maendeleo na jamii ya kimataifa kuhusiana na matukio yanayoshuhudiwa nchini yanayohatarisha kanuni za kidemokrasia na kuchochea migawanyiko.

Wakizungumza na Taifa Leo Jumatatu, jamii ya Wakenya katika mataifa ya kigeni imeelezea wasiwasi wake kuhusu kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kuendelea kuchelewesha tume mpya ya uchaguzi na pendekezo la kuongeza muda wa mihula ya rais na wabunge.

Kundi hilo linalofahamika kama Disporians Against Corruption in Kenya (DACK) limekashifu vikali matukio ya hivi punde kisiasa yanayoshuhudiwa nchini wakionya hatua hizo za serikali wanazosema “ni kinyume na katiba na demokrasia” zinatishia kuhujumu kanuni za demokrasia na kuhatarisha taifa.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa DACK, Ben Ateku, wamekosoa mchakato wa kumfurusha Naibu Rais ulioendeshwa kwa kasi ya ajabu, chini ya wiki moja, na bunge la kitaifa na seneti.

Wanahoji kuwa hatua hiyo imechochewa kisiasa na serikali ya Kenya Kwanza kwa madhumuni ya kujiimarisha mamlakani.

“Kubanduliwa kwa Naibu rais sio tu kumshambulia mtu binafsi anayeshikilia afisi bali ni ishara tosha ya hali ya chama tawala kukosa kuruhusu maoni tofauti,” alieleza Bw Ateku.

Isitoshe, Wakenya hao wanaoishi ulaya wamehoji sababu ya nchi kukosa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wakisema ni njama ya viongozi waliopo kuendelea kudhibiti na kulemaza demokrasia.

Rais William Ruto alitia saini kuwa sheria Mswada wa Marekebisho kuhusu IEBC 2024 akiahidi kuharakisha mchakato wa kuunda tume mpya ya uchaguzi na kumteua mwenyekiti na makamishna.

Hata hivyo, uamuzi wa korti Septemba uliosimamisha uteuzi wa wanachama wa jopokazi la uteuzi, ulivuruga mchakato huo na kusababisha ucheleweshaji zaidi.

IEBC haijakuwa ikifanya kazi ipasavyo tangu Januari mwaka uliopita wakati aliyekuwa mwenyekiti Wafula Chebukati alipojiuzulu.

Kulingana na mkurugenzi wa mawasiliano DACK, Steve Mbugua, ucheleweshaji wa IEBC unazua maswali ikizingatiwa unajiri wakati Wakenya wengi wamepania kuwarejesha nyumbani wabunge wao waliopiga kura kumfurusha Naibu Rais na kupitisha Mswada wa Fedha 2024 uliofutiliwa mbali.

“Kukosa tume mpya ya uchaguzi miezi kadhaa baada ya idadi kubwa ya Wakenya kuashiria nia ya kuwafuta kazi viongozi wao ni jambo la kutiliwa shaka na linapaswa kumshughulisha kila Mkenya,” alisema Bw Mbugua.

“Hatua hiyo inazua masuali kuhusu haki na uhuru wa chaguzi zijazo.”

Kuhusu suala la kuongeza muda wa mihula ya afisi ya rais na viongozi wengine wanaochaguliwa hadi miaka saba kutoka miaka mitano ya sasa, kundi hilo limekashifu vikali hatua hiyo.

Mswada wa Kufanyia Marekebisho Katiba ya Kenya uliowasilishwa na Seneta wa Kaunti ya Nandi, Samson Cherargei, unalenga kuongeza muda wa hatamu za uongozi kwa miaka miwili.

Wanahoji kuwa hatua hiyo “ni jaribio la kukwamilia mamlaka na kulemaza maendeleo ya kidemokrasia ambayo Kenya imefanikisha kwa miaka mingi.”