Jamvi La Siasa

Wakazi Mlima Kenya walivyoondoka hotuba ya Ruto ikisomwa siku ya Mashujaa

Na WAANDISHI WETU October 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 3

WAKAZI wa Mlima Kenya Jumapili Mashujaa walionyesha maasi ya wazi dhidi ya Rais William Ruto kufuatia kutimuliwa kwa naibu wake Rigathi Gachagua wakati wa sherehe ya Mashujaa.

Katika kaunti za ukanda huo wakazi hawakujitokeza katika sherehe hizo huku viongozi waliochaguliwa wanaompinga Bw Gachagua pia wakikosa kuhudhuria wakihofia kuzomewa.

Magavana wengi walisusia sherehe hizo kinyume na hapo awali ambapo walizitumia kuorodhesha ufanisi wao. Magavana kutoka kaunti za Nyeri, Murang’a, Isiolo, Meru, Tharaka Nithi na Embu hawakujitokeza huku sherehe hizo zikiongozwa na manaibu gavana, maafisa wa utawala na makatibu wa kaunti.

Katika Kaunti ya Murangá ni watu wa kuhesabiwa tu walifika na walianza kuondoka hotuba ya rais ilipoanza kusomwa. Wabunge nao walikosa kufika wakihofia ghadhabu za raia kutokana na masaibu ya Bw Gachagua.

Sherehe za Murangá ziliandaliwa kwenye uga wa Ihura zikiongozwa na Kamishina wa kaunti Joshua Nkanatha ambapo ni chini ya watu 50 walihudhuria wengi wao wakiwa maafisa wa serikali.

Wakazi waliondoka mmoja baada ya mwengine Bw Nkanatha alipoanza kusoma hotuba ya Rais Ruto.

“Kama Rais angekuwa hapa binafsi ningemzomea na kuondoka kwenye mkutano wake. Amefanya maisha yetu yawe magumu na bado anahangaisha Gachagua,” akasema mkazi Martin Nduati, 28.

Katika uga wa Kangangu, wakazi waliondoka Naibu Kamishina Gitonga Murungi alipoanza kusoma hotuba ya Rais.

“Nilikuja hapa ili hotuba yake ikianza kusomwa niende zangu. Anacheza siasa mbaya na anastahili kuondolewa madarakani pia,” akasema Mzee Warui Njuguna, 78.

Seneta wa Murangá Joe Nyutu, mwandani wa Bw Gachagua alisema kuwa hakuwa na haja ya kuhudhuria sherehe hizo kwa sababu ya siasa za Rais dhidi ya naibu wake.

“Hata ukiangalia hotuba yake, alikuwa akikejeli ukanda wa Mlima Kenya. Hata alidharau Mau Mau kwa kudai eti uhuru wa Kenya ulipigiwa na Wakenya wote na huo si ukweli,” akasema Bw Nyutu.

Mbunge wa Maragua Mary wa Maua ambaye huwa hakosi kuhudhuria sherehe hizo alisema anasubiri kusherehekea Krismasi pekee kwa sababu Rais ameonyesha ni kiongozi katili aliporuhusu naibu wake aondolewe mamlakani akiwa hospitalini.

Katika uga wa Ruringu Kaunti ya Nyeri, viti vingi vilikuwa wazi huku vichache vikikaliwa na maafisa wa usalama na viongozi wa dini.

Kwenye uga wa Dedan Kimathi, Naibu Kamishina wa Nyeri ya Kati Joseph Mwangi aliamua kuwaita makundi ya kutumbuiza wakalie viti ambavyo vilikuwa wazi. Wanasiasa nao walisusia hafla hiyo na Bw Mwangi aliposimama kusoma hotuba ya rais, waliokwepo walianza kuenda zao.

Kwenye Kaunti ya Meru, Gavana Kawira Mwangaza hakufika katika Chuo cha Kiufundi cha Meru huku akiwakilishwa na Katibu wa Kaunti Kiambi Atheru. Hafla hiyo ilihudhuriwa na watu wachache sana.

Hali ilikuwa hiyo hiyo Tharaka Nithi ambapo sherehe za Mashujaa ziliongozwa na Kamishina wa kaunti David Gitonga huku mbunge wa Tharaka Gitonga Murugura akihudhuria pia japo alikwepa kuzungumzia masaibu ya Bw Gachagua.

Katibu wa Kaunti ya Isiolo Dadhe Boru na Kamishina wa kaunti Geoffrey Omoding walihudhuria sherehe zilizofanyika Isiolo.

Katika Kaunti ya Embu sherehe za Mashujaa ziliongozwa na Naibu Gavana Kinyua Mugo na Kamishina wa Kaunti Jack Obuo.

Wabunge Eric Muchangi (Runyenjes), Gitonga Mukunji (Manyatta), Geoffrey Ruku (Mbeere Kaskazini) na Nebart Muriuki (Mbeere Kusini) hawakufika uga wa Karairu kuhudhuria Mashujaa wala hawakutuma udhuru.

Kwenye gatuzi la Kirinyaga wabunge Mary Maingi (Mwea), George Kariuki (Ndia), Gichimu Githinji (Gichugu) na Gachoki Gitari (Kirinyaga ya Kati) hawakufika  uga wa Ndindiruku.

Mnamo Ijumaa Mbunge wa Igembe Kaskazini Julius Taituma alijipata pabaya alipozomewa na walimu, alipojaribu kutetea kuondolewa mamlakani kwa Gachagua. Alikuwa amehudhuria mkutano wa Chama cha Walimu Nchini (KNUT) tawi la Meru.

Gavana Joshua Irungú wa Laikipia alilazimika kuwaomba raia watulie ili Kamishina wa kaunti Onesmus Kyatha asome hotuba ya rais katika uga wa Rumuruti.  Viongozi wengine waliochaguliwa nao walihepa sherehe hizo.

“Tutulie tukisubiri jinsi suala la Gachagua litakavyoamuliwa. Hapo kuna makabila yote na tukianza chuki basi ghasia zitazuka,” akasema Bw Irungu.

Kwenye uga wa Kanyoni, umbali kidogo kutoka mji wa Nanyuki wakazi walikuwa wakija kufuatilia hafla kisha kutoweka na kurudi tena. Walifanya hivyo wakisubiri mlo wa bure ambao ulikuwa ni kitoweo cha nyama na mchele.

Nyumbani kwa Bw Gachagua, eneobunge la Mathira, mbunge wake Eric Wamumbi hakujitokeza. Sherehe ambazo ziliandaliwa katika kituo cha kibiashara cha Kiamabara, mita chache kutoka kwa boma la Bw Wamumbi pia ilikuwa na wakazi wachache mno.

Ripoti za MWANGI MUIRURI, MWANGI NDIRANGU, STEPHEN MUNYIRI, GEORGE MUNENE, DAVID MUCHUI na JOSEPH KANYI