Kimataifa

Trump kifua mbele miongoni mwa Waarabu wapiga kura Amerika

Na MASHIRIKA October 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MICHIGAN, AMERIKA

ZIKISALIA wiki mbili pekee kabla ya uchaguzi kufanyika, aliyekuwa Rais wa Amerika Donald Trump anaonekana kuwa kifua mbele miongoni mwa Waarabu ambao ni wapiga kura katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi duniani.

Vita vinavyoendelea kwenye ukanda wa Gaza vinaendelea kugharimu Democrats ambao mwaniaji wao ni Makamu wa Rais, Kamala Harris.

Trump, ambaye alikuwa rais wa Amerika kati ya 2016-2020, anaongoza kwa asilimia 45 dhidi ya asilimia 43 za Harris miongoni mwa Waarabu ambao ni wapiga kura Amerika.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mashirika kadhaa yanayotangaza habari kwa Kiarabu, zikiwa zimesalia wiki mbili kabla kura zipigwe, Trump anapendelewa na Waarabu Wamarekani.

Kati ya sababu ambazo zimefanya Trump achangamkiwe ni kuwa anaonekana kama mwaniaji ambaye ana uwezo wa kutatua ugomvi kati ya Israel na Palestina kwenye Ukanda wa Gaza.

Asilimia 39 ya Waarabu wanaamini kuwa Trump anaweza kuleta utulivu ukanda wa Gaza ikilinganishwa na asilimia 33 za Harris.

Hata hivyo, wawili hao wote wana asilimia 38 kwenye suala la kiongozi yupi bora wa Amerika kwa mataifa ya ukanda wa Mashariki ya Kati.

Asilimia 29 ya wapiga kura Waarabu wanasema kuwa suala la ugomvi katika Ukanda wa Gaza ndilo litaamua mkondo watakaoupigia kura kwenye uchaguzi huo wa Novemba 5.

Asilimia 21 wanaamini ni uchumi na gharama ya maisha huku asilimia 13 wakisema ni ubaguzi wa rangi na ubaguzi kwenye nyanja nyingine serikalini.

Licha ya kuonekana kuwa kifua mbele, Trump anaonekana vilevile kuunga utawala wa sasa wa Israel ikilinganishwa na Harris ambaye amekuwa akikoselewa kwa kushirikiana na Rais Joe Biden kuhakikisha Israel inawaangamiza Wapalestina.

Matokeo ya kura hizo za utafiti ni dalili za hivi punde kuonyesha kuwa hatua ya Rais Biden kuunga Israel kwenye vita vinavyoendelea Ukanda wa Gaza kunadidimiza matumaini ya Harris kumbwaga Trump mnamo Novemba 5.

Mapema mwezi huu, Taasisi ya Waarabu Amerika ilitoa matokeo ambayo yalimweka Trump mbele kwa asilimia 42 dhidi ya asilimia 41 ya Harris.

Takwimu zinaonyesha kuwa Harris yupo chini sana katika uungwaji mkono miongoni mwa wapiga kura Waarabu kuliko jinsi Biden alivyokuwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2020.

Kati ya majimbo ambayo huenda yakaamua matokeo ya kura Amerika ni Michigan ambapo wapiga kura Waarabu wapo wengine sana.

Mnamo Septemba, Meya wa Michigan, Hamtramck, alimuidhinisha Trump na kumrejelea kama mwanaume mwenye sera ambaye atalainisha utawala wa Amerika.

“Iwapo Kamala atapata miaka minne ya uongozi, basi ukanda wa Mashariki ya Kati utaendelea kuungua kwa muda wa miaka minne ijayo,” akaongeza.

“Watoto wenu watakuwa wanahangaika vitani na huenda kukazuka Vita vya Tatu vya Dunia. Haya yote hayatafanyika iwapo Trump atakuwa Rais wa Amerika,” akasema Trump mnamo Jumatatu.