Habari za Kitaifa

Gachagua ajipeleka binafsi mahakamani kupigania wadhifa wake

Na RICHARD MUNGUTI October 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NAIBU Rais aliyetimuliwa Rigathi Gachagua Jumanne alihudhuria kikao cha Mahakama Kuu wakati wa kusikizwa kwa kesi mbili za kupinga kuondolewa kwake mamlakani.

Bw Gachagua alifika katika Mahakama ya Milimani jijini Nairobi akiwa na msafara wa magari sita akiandamana na Mbunge wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru, almaarufu Major Donk, aliyekuwa Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala na mawakili kadhaa.

Kulikuwa na  maafisa wengi wa usalama katika majengo ya mahakama na hata ndani ya  mahakama.

Walipofika mbele ya majaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Freda Mugambi, mawakili wa Bw Gachagua, wakiongozwa na Wakili Mkuu Paul Muite, walisema hawakuwa kortini kwa hiari yao.

Mahakama ilieleza kuwa faili za kesi zilitumwa kwa Jaji Mkuu mnamo Oktoba 18 na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu akateua majaji kusikiza kesi hizo.

Jaji Mrima alisema kesi hizi ziliwasilishwa kupitia mtandao na majaji wakaagiza zitajwe leo.

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA