Jamvi La Siasa

Siasa za usaliti na ‘njama za mauaji’ zarejea kwa kishindo Kenya

Na COLLINS OMULO October 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SIASA za madai ya usaliti na njama za watu kuuawa zimeanza kujitokeza tena baada ya naibu rais aliyetimuliwa mamlakani kudai alijaribiwa kulishwa sumu mara mbili.

Akihutubu Jumapili baada ya kuondoka Hospitali ya Karen, Nairobi, Naibu Rais aliyetimuliwa mamlakani alidai kuwa kulikuwa na majaribio mawili ya kuumua mnamo Agosti 30 kupitia kuwekewa sumu kwenye mlo.

Jaribio la kwanza, alidai, lilitokea kwenye hoteli ya Acacia, Kisumu akiwa kwenye ziara ya kisiasa eneo la Nyanza. Alidai kuwa kulikuwa na jaribio jingine mnamo Septemba 3 wakati ambapo chakula alichostahili kula kwenye mkutano na Baraza la Wazee wa Agikuyu pia kilitiwa sumu.

Bw Gachagua ambaye anapambana mahakamani kuhakikisha kuwa habanduliwi kabisa mamlakani, pia alimwendea Rais akimtaka akome kuhangaishwa familia yake wala asiwaue watoto wake.

“Inasikitisha kuwa Rais ameamuru nipokonywe walinzi wakati ambapo nipo hospitalini. Sina afisa yeyote wa polisi hapa na ameamrisha hata wale ambao walikuwa nyumbani kwangu Nyeri na hapa Karen waondolewe,” akasema Bw Gachagua.

“Sikujua Rais angekuwa katili hivi dhidi yangu. Nimepigwa na mshangao mwanaume ambaye nilimsaidia kupata mamlaka amenigeuka na ananifanyia haya wakati ambapo napigania uhai wangu hospitalini,” akaongeza Bw Gachagua.

Hii si mara ya kwanza ambapo maadai ya mauaji na kuhangaishwa kwa familia ya mwanasiasa zimeanza kuchipuka. Bw Gachagua alikuwa anaonekana kufuata mkondo wa bosi wake ambaye alitoa madai kama hayo wakati ambapo uhusiano wake na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta uliingia mdudu, wawili hao wakiwa mamlakani.

Mnamo Julai 2022, Rais Ruto wakati huo akiwa naibu rais alimwaambia Bw Kenyatta akome kutumia vitisho dhidi yake baada ya kumuidhinisha Kinara wa Azimio Raila Odinga kama mgombeaji wa urais aliyekuwa akiunga kwenye kura ya mnamo Agosti 2022.

Rais Ruto wakati huo alidai kulikuwa na njama ya kumuua pamoja na wanafamilia wake na wandani wake wa kisiasa. Alidai kuwa Bw Kenyatta aliandaa mkutano wa kibinafsi ambapo alimtishia pamoja na wandani wake na akamtaka asielekeze hasira zake kwa watoto wake.

“Namwambia Rais akome kuwatishia watu kwa sababu kazi yake ni kuhakikisha kuna amani nchi. Akome kutuambia kuwa tutajua wewe ndiye rais na kutuhangaisha kwa sababu hatuwezi kutishika,” akasema Ruto wakati huo.

“Mradi tu usiwaue watoto wangu, mimi nitakukabili lakini tuheshimiane,” akaongeza.

Rais Ruto alitoa madai hayo baada ya Bw Kenyatta kumrejelea kama mwanasiasa mwongo ambaye hakuwa amekomaa kisiasa na akawataka wapigakura wamuunge Raila.

“Bw Rais koma kuzungumza kunihusu na uzungumzie mwaniaji wako. Nilikuunga mkono wakati ulihitaji mtu wa kukusaidia kama hutaki kuniunga mkono, niache,

“Nataka nimwambie Rais kuwa licha ya kunifanyia haya yote, sitalipiza kisasi kwa sababu mimi ni Mkiristo. Nitahakikisha umestaafu kwa amani na uniache niongoze nchi kwa sababu najua kile nafanya,” akasema Rais Ruto wakati huo.

Bw Kenyatta hata hivyo alimjibu akisema kuwa Ruto alikuwa amemhangaisha na kumtusi kwa miaka mitatu wala angekuwa na nia ya kumuumiza angekuwa ashafanya hivyo.

“Miaka hiyo mitatu si nimekuwa nikishikilia afisi hii na nilikuwa na mamlaka yote. Wakati huu ambapo nastaafu na sina mamlaka ndiyo unafikiria nina muda wa kukutafuta?” akasema Bw Kenyatta.

Mwaka moja baadaye, Bw Kenyatta naye baada ya kustaafu alidai Rais Ruto alikuwa akimhangaisha na kulenga familia yake. Akizungumza bomani mwa mwanawe mkubwa Jomo Muigai mtaa wa Karen, Bw Kenyatta aliitaka serikali ikome kulenga familia yake na imkabili moja kwa moja.

“Wanafaa waniambie wanataka nini kwa watoto wangu kwa sababu wamewapokonya walinzi na sasa wanataka kuchukua silaha ambazo wanazo kihalali. Ni kwa sababu wanapanga kitu?

“Kama wanapanga jambo basi wasilenge watoto wangu au mamangu. Wapange dhidi yangu na waache familia yangu kabisa,” akasema Bw Kenyatta.

Alilaumu serikali ya Rais Ruto kwa kushiriki njama ya kumhangaisha na familia yake baada ya kuwapokonya walinzi. Alisema serikali inastahili kumwendea na kulipiza kisasi cha kisiasa naye badala ya kulenga familia yake.