Habari za Kitaifa

Naibu Rais au Waziri wa Usalama? Kindiki akosa kufika mbele ya maseneta kujibu maswali kuhusu wizara

Na COLLINS OMULO October 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MKANGANYIKO kuhusu nani ndiye Naibu Rais halali jana ulijitokeza katika Seneti baada Naibu Rais Mteule Kithure Kindiki, ambaye amekuwa akihudumu kama Waziri wa Usalama, kufeli kufika mbele ya bunge hilo.

Haya yalijiri baada ya Profesa Kindiki kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa wiki jana kuchukua mahala pa Rigathi Gachagua aliyetimuliwa na Seneti mnamo Oktoba 17, 2024.

Profesa Kindiki alikuwa ameratibiwa kufika mbele ya kikao cha asubuhi cha Seneti jana, Jumatano, kujibu maswali kutoka kwa maseneta yaliyoelekezwa kwa Wizara ya Usalama wa Ndani.

Hata hivyo, Spika wa Muda Hillary Sigei (seneta wa Bomet) alisema alipokea barua kutoka kwa Profesa Kindiki akiomba radhi kwamba hangefika, ombi ambalo Kamati ya Kuratibu Shughuli za Seneti liliidhinisha.

“Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala ameomba kuwa hangefika katika bunge hili ilivyoratibiwa. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote uliosababishwa na hali hii,” barua hiyo inasema.

Kulingana na ratiba ya shughuli za Seneti, mawaziri Profesa Kindiki na Opiyo Wandayi, ambaye pia hakufika, waliratibiwa kufika jana kujibu maswali kutoka kwa maseneta.

Barua kutoka kwa Profesa Kindiki haikutoa sababu iliyochangia kutofika kwake katika Seneti, ishara ya wingu la mkanganyiko linalogubika cheo anachokishikilia wakati huu.

Kwa upande wake Waziri wa Kawi Bw Wandayi, katika barua yake kwa Seneti alisema hangeweza kufika kwa sababu amesafiri ng’ambo kwa shughuli za kikazi, zilizoanza Oktoba 22 hadi Oktoba 24, 2024.

“Tunasikitika kuomba kuahirishwa kwa mkutano ulioratibiwa kufanyika Oktoba 23. Waziri amesafiri nje ya nchi kwa shughuli rasmi za kikazi zitakapodumu kati ya Oktoba 22 hadi 24, 2024. Tunaomba kuwa mkutano huo ufanyike tarehe nyingine itakayowafaa,” ikasema barua kutoka kwa afisi ya Bw Wandayi.

Kiranja wa Wengi katika Seneti Boni Khalwale aliibua mjadala kuhusu sababu iliyochangia Profesa Kindiki kufeli kufika akieleza kuwa hadhi yake imebadilika kutoka kuwa Waziri wa Usalama hadi Naibu Rais kufuatia kuidhinishwa kwake uteuzi wake na Bunge la Kitaifa.

“Nimevutiwa na barua kutoka kwa Wizara ya Usalama wa Ndani kwamba hangefika mbele ya Bunge hili. Lakini ni bunge hili lililoidhinishwa kuondolewa afisini kwa aliyekuwa Naibu Rais na baadaye Profesa Kindiki akaidhinishwa kama Naibu Rais Mteule,” akaeleza Dkt Khalwale ambaye ni Seneta wa Kakamega.

“Kwa hivyo, kwa mtazamo wa Bunge, Naibu Rais wa Kenya ni Kindiki. Ningependa kurai sekritariati kukoma kufanya kazi ya bure kwa kumtumia mialiko ili aje kujibu maswali yaliyoelekezwa kwa Wizara ya Usalama. Ikiwa mnayo maswali yoyote kwake, mmwalike aje kuzungumzia masuala yanayohusu afisi ya Naibu Rais,” Kiranja huyo wa wengi akaongeza.

Seneta wa Embu Alexander Mundigi aliunga mkono kauli ya Dkt Khalwale, akiongeza kuwa: “Tuko na Naibu Rais kwa jina Kindiki. Hangekuja hapa kama Waziri wa Usalama. Wale wanaojiita watu wa Mlima Kenya Magharibi sharti wajue kuwa tuko katika katika serikali inayoshirikisha mirengo yote; hamna migawanyiko kwa misingi ya vyama.